Monday, December 10, 2012

Ubabu waukataa



Ubabu waususia, kuwa waliotakiwa,
Yao wahangaikia, yanayowaigizia,
Nusura hawajafikia, kwingine watarajia,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

Leo waiangalia, sio kesho kuhofia,
Mambo wakapangilia, usalama kuuzua,
Yao wameshikilia, muhimu yaliyokuwa,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

Ya watu wanaambiwa, si tena kujionea,
Sifa wanapelekewa, kashfa zawaambaa,
Maamuzi wakitoa, sahihi wajidhania,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

Wasifa wajifukia, wajihi ukabakia,
Tabasamu walotoa, labaki kuning'inia,
Madubu waliokuwa, mifereji wachimbua,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

Wamekuwa wote sawa, na waliotangulia,
Ziro walijipandia, sifuri wajivunia,
Rahma imetulea, yeyote angejaliwa,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

Tofauti haijawa, kuiona Tanzania,
Bahati waliovua, samaki wajiozea,
Kilema kinachanua, huku meno waachia,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

Nta waliyotumia, inayeyuka kwa jua,
Moto wanaikokea, chini pia kuitia,
Hali wanaangalia, maajabu kutokea,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

Yao waliyoanzia, ndiyo yanaendelea,
Vingine haitakuwa, afueni kutokea,
Mbele hawakufikiria, nyuma waliangalia,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

Yetu walipotumia, haya hawakuotea,
Mbio walizokimbia, ndipo hapa zaishia?
Ni nani asiyejua, mzizi wanaung'oa,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

Njama wamekusudia, kufa na mtu walia,
Kwalo hawatatulia, hadi yakiwafikia,
Mola awaangalia, yake ameshaamua,
Ubabu waukataa, yao kushughulikia!

No comments: