Saturday, December 29, 2012

Mpaji na mnyang'anyaji

NDIYE mwenye kugawiwa, wengi wasema kutoa,
Kisha akaja kutwa, vyake akavihukua,
Nani wa kumchezea, sahihi aliyekuwa ?
Mpaji na mnyang'anyaji, huyo huyo si mwingine !

Ni mwepesi wa kutoa, kiumbe ukajaliwa,
Nyota yako juu kuwa, ikunukuu dunia,
Wajibuo ukijua, hapo waweza bakia,
Mpaji na mnyang'anyaji, huyo huyo si mwingine !

Mrahisi kuachia, kama ya kushikilia,
Weye kujishtukia, chini unaangukia,
Na unapotumbukiwa, humohumo ukakaa,
Mpaji na mnyang'anyaji, huyo huyo si mwingine !

Akiependa kwa ridhaa, aweza akakutoa,
Fursa kukuachia, upendavyo kutumia,
Ukawa wako wasaa, kuzama au kupaa,
Mpaji na mnyang'anyaji, huyo huyo si mwingine !

Wengi wanapogawia,  huanza kujizuzua,
Njia wakaiachia, na kuingia nazaa,
Pasina ya kuelewa, kwao hakuna wasaa,
Mpaji na mnyang'anyaji, huyo huyo si mwingine !

Na anavyoshudhudia, kifua mnakiinua,
Pindi mnapojaliwa, mazuri yanu yakawa,
Mkawa mwajisifia, yeye awapendelea,
Mpaji na mnyang'anyaji, huyo huyo si mwingine !

Kikija kuondolewa, hamtoacha kulia,
Udhalili kawatia, wapi mtakimbilia,
Kama vile mwajijua, nyie wa juu tu kukaa,
Mpaji na mnyang'anyaji, huyo huyo si mwingine !

Wajane hamkuwafaa, na yatima mwakimbia,
Masikini nao pia, yenu waliyahofia,
Hivi mkijichungua, haki  hamjatendewa ?
Mpaji na mnyang'anyaji, huyo huyo si mwingine !

Kadari tungeliijua, hivi tusingelikuwa,
Mengi tungeyaachia, na  machache kufatia,
Wengi tunachokimbilia, wala hatutachukua,
Mpaji na mnyang'anyaji, huyo huyo si mwingine !

No comments: