Tuesday, December 11, 2012

Jirani yangu mchawi

MSHIRIKINA najua, wala sio kuambiwa,
Mimba uliichawia, kifo ukitarajia,
Hilo likagunguliwa, mchana kukuumbua,
Jirani yangu mchawi, salama nakuombea!

Visenti waokotea, mchawi kumgawia,
Hivi nikishaumia, nini utajipatia?
Kitabu nakifungua, dua ninakuombea,
Jirani yangu muongo, ukweli nakuachia!

Ubaya ukinitakia, salama nakuombea,
Ndumba ukinitupia, ubani nitakuchomea,
Hiliki ukiizua, kulaki kazi ikawa,
Jirani yangu mchawi, salama nakuombea!

Uongo ukiizua, ukweli nitakugea,
Shimo ukilichimbua, mimi nitalifukia,
Haki ukiinunua, maradufu nalipia,
Jirani yangu muongo, ukweli nakuachia!

Mke ukimmendea, mie nitakuachia,
Maruhani watakiwa, hata hivyo kuondoa,
Wasije kuparamia, uhai ukapotea,
Jirani yangu mzinzi, mke nimekuachia!

Mwizi ukiniibia, namimi nikakujua,
Milango nitafungua, urahisi kukupatia,
Njoo uje kuchagua, vizuri ukachukua,
Jirani yangu jambazi, milango nimefungua!

Husuda uliyejaa, ndani hebu karibia,
Mali ukijionea, na wewe pia chagua,
Tabaka ninazijua, haya budi kutokea,
Jirani yangu hasidi, mali yangu nakwachia!

Mnafiki ulokuwa, fitina zimekujaa,
Kilinge nakuachia, utakayo kuongea,
Ila ukimalizia, ububu utauvaa,
Jirani yangu mnafiki, uchamungu nakwombea!

Uliyejaa ubaya, ghasia kunifanyia,
Kelele kunipigia, usingizi ukiingia,
Upole nakuachia, uweze kuuzoea,
Jirani yangu mbaya, uzuri nakuachia!

Ukubwa uliyopewa, na pua kunikunjia,
Huo nimekuachia, mimi moto nahofia,
Pengine umejaliwa, peponi utaingia,
Jirani yangu mkubwa, ukubwao siutaki!

Mlozi uliyekuwa, na Kongo unatokea,
Au Mmanyema kuwa, Kigoma unatokea,
Au kama ni Makua, kusini umezaliwa,
Jirani yangu mlozi, salama nakuombea!

Uchoyo sijaujua, tokea kujitambua,
IKiwa umeishia, ndio kisa kuchawia,
Lipi la kukuachia, kwalo ukaliridhia?
Jirani yangu muongo, ukweli nakuachia!

Kama wataka tanua, vitu nyumbani kujaa,
Milango ninafungua, utakavyo kuchukua,
Pengine utatulia, hamuyo ikipungua,
Jirani yangu jambazi, milango nimefungua!

Kufulia walilia, chini mimi kujikwaa,
Wewe juu ukapaa, anga ukalifikia,
Bssi mimi najiachia, wewe kuendelea,
Jirani yangu hasidi, mali yangu nakwachia!

Hesabu ikitimia, wewe utaniambia,
Mazao ukishapewa, nijazie na gunia,
Ukumbusho likakaa, tafsiri ya dunia,
Jirani yangu mnafiki, uchamungu nakwombea!

Au kaziyo kuua, uhai kukatishia,
Ndilo walifurahia kuwa wewe wabakia,
Kufa utanifatia, kama ninatangulia,
Jirani yangu mzinzi, mke nimekuachia!

Ninamuenzi Jalia, wachawi anayejua,
Falaq katupatia, kusoma kama dua,
Kila yakizingatiwa, wachawi wakaelea,
Jirani yangu mbaya, uzuri nakuachia!




No comments: