Monday, December 10, 2012

Akaaye kileleni



NAONA kama utani, na mzaha kubaini,
Udhaifu na uduni, unaokosa mizani,
Lugha hatuelewani, ndimi hazina makani,
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Apandaye kileleni, mkono akushikani,
Hali unashuka chini, lifti haimo kzini,
Utadhani majinuni, huruma kuwa hisani.
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Mushkeli naamini, lilo maana sioni,
Maisha ya dhadhi gani, na mlo haubaini,
Wao vyajaa mezani, ufukara hawaoni,
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Kauli wasikizeni, zipitapo sikioni,
Ila msiwaamini, yao si ya udhamini,
Wajaziwa makapuni, nanyi hammo machoni,
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Habari zao uani, hazitoki barazani,
Waambiwa ya puani, hayaendi sikioni,
Hawajui kitu gani, chatafuna kitandani,
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Hata kwao ni shakani, kama kweli wabaini,
Wasikiza mtaani, nyuzi zende redioni ?
Kisha zina wadhamini, wanyonyaji wa mwandani?
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Ya kwao sio kanuni, yanatangazwa ilani,
Wachuma ya maskini, na wakwasi kuwawini,
Wana na wanandani, ndio wapewa hisani?
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Magenge wayabaini, kuuliza bei gani,
Watu wakawazaini, eti kugura chamani,
Mizizi i mashakani, imepotea njiani,
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Hawayajui ya chini, waishio ghorofani,
Hiyo siyo yao fani, usanii waamini,
Wapewa ya mdomoni, wakayaweka moyoni ?
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Kauli pasi thamani, zatangazwa hadharani,
Wakacheka wanandani, ukweli wanaobaini,
Jambo hili jambo gani, si mkia si kichwani?
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?

Macho yaangazeni, kwingineko duniani,
Usanii kubaini, ulivyojaa nchini,
Wengine wako angani, sisi tuko ardhini?
Akaaye kileleni, hivi ajua ya chini?



No comments: