Monday, December 24, 2012

D O L A

USHABIKI wa kijinga, zama zake zaishia,
Watu sasa wanachanga, yenye hoja kuchengia,
Si rahisi kuwavunga, njia wakazifungua,
kodi yajenga taifa, toka lini kiwe chama ?
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Uongo wakiizua, ukweli watajibiwa,
Hakuna asiyejua, kodi yajenga dunia,
Wao wakituambia, vingine hatutajua,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Yeyote anayekuwa, dola ameichukua,
Hukusanya kikajaa, kisha akakitumia,
Kula haiwi ridhaa, ila watu kuwafaa,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Wao inaelekea, huanza kwa kujilia,
Kisha wakavigawa, kwa ndugu pia jamaa,
Kidogo kinachobakia, ndio wakatuhadaa,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Vikubwa vingelikuwa, vyema ingelitumia,
Kodi tuliyoitoa, wala ndogo haikuwa,
Ujanja wametumia, bianfsi kuwafaa,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Kwa uongo kuutia, ndio watu wachukia,
Ukweli mkiutoa, watu watawaelewa,
Mlavyo mmejaliwa,nafasi mliyokaa,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Ila si kutuambia, wengine watafulia,
Kazi hawataijua,ila mliojaliwa,
Ndio tu mnaelewa, hazina kusimamia,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Kama hivyo kungekuwa, vipi nako kwaibiwa,
Milango mmefungua, au chama kujifaa,
Mbona mwagugumia, ukweli hatujajua ?
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Uongozi si sanaa, ujuzi unatakiwa,
Na kila mwenye kujua, siasa alielewa,
Vingine haitakuwa, ila kwa wanaoelwa,

Ila kwa wanaoelwa,  watakao kuimbiwa,
Mapambo wakapambiwa, matapishi yamejaa,
Kinyqa kisipokuwa, maajabu hutokea,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Kodi dereva ikiwa, nchi inatengamaa,
Udhibiti usopwaya, malengo yakatimia,
Watu wakajisema, nchi yenyewe yakuwa,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Kodi ikishachezewa, haliwi hata la kuwa,
Kila kitu kitapwaya, na chuki zikaanzia,
Wenyewe kujiibia, hayo huwa yatokea,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Uswizi zinazokaa, watu hazijawafaa,
Huenda wakajifia, kisha bure kupotea,
Na wana kuwa vichaa, zikashindwa kuwalea,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Batili ikitumiwa, mtenzi anaumia,
Awali hakuyajua, ukubwani hutokea,
Macho akifungulia, roho akaagulia,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Haki ya mtu kuliwa, hilo halijaruhusiwa,
Kuna siku huwadia, deni kwenda kulipiwa,
Kama baba haikuwa, wana wake itakuwa,
Kodi yajenga taifa, toka lini iwe dola ?

Tamaa waliojaa, kidogo wakipokea,
Kikubwa hukiachia, kikaenda kupotea,
Yao wakaangalia, si yetu kutulindia,
Kodi yajenga taifa, toka lini kiwe dola ?

Kumbe kinachotokea, ni kama kupotezea,
Wakuu wakishapewa, ni ruhusa kupotea,
Udhibiti twafulia, bado tunashangilia ?
Kodi yajenga taifa, toka lini kiwe dola ?

Hazina inachopokea, hivi nusu chafikia,
Mwakyembe akitua, mbona kingi chavuliwa ?
Nini kinachotokea, mbona hamjatwambia,
Kodi yajenga taifa, toka lini kiwe dola ?

Hivi kadi ya Slaa, ni mazito kuliko haya,
Chama mnatuhumiwa, mashamba ya bibi kunywea,
Au hamjasikia, huko mnakopitia ?
Kodi yajenga taifa, toka lini kiwe dola ?

Itajengwa Tanzania, fedha zisipopotea,
Nyie mnaziachia, watu waenda chezea,
Mtu milioni mia, kwa siku moya azoa ?
Kodi yajenga taifa, toka lini kiwe dola ?

Marudufu yakitua, kisha vyema kutumiwa,
Itafufuka Tanzania, na kisha kuanza kupaa,
Hapo stahi itakuwa, sasa kuanza sifiwa,
Kodi yajenga taifa, toka lini kiwe dola ?

Kujipanga yatakiwa, tena haraka ikawa,
Kizidicho kuingia, wachache kutojilia,
Kumbe tulichojaliwa, wote chaweza tufaa ?
Kodi yajenga taifa, toka lini kiwe dola ?

No comments: