Monday, December 24, 2012

Hapa ninapoishia



TONGOTONGO wazitoa, kushoto pia kulia,
Uso sasa wananawa, uchafu kutobakia,
Mengi yamewaingia, inshallah watakuwa,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Hadidu zake rejea, nyuma nilikoanzia,
Jengine halijakuwa, bali ni demokrasia,
Kuitunza na kukua, nchini ikaenea,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Njia nawasafishia, wasiweze kupotea,
Na mipaka kuitia, nje wasende ingia,
Mkaza wakiijua, haki watajilindia,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Kitu sikuaramia, walal cha mtu kutwaa,
Kwingine nimekimbia, ardhi kuwaachia,
Watu wengine wabaya, nao si vyema kukaa,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Mbali nimekimbilia, wanako nikumbatia,
Pasina kitu kutoa, ni akili kuchangia,
Yangu wakayaelewa, yaweza kusaidia,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Mola ninamsabilia, apate nifagilia,
Kanionyesha njia, salama nikapitia,
Hadi kwenda kufkia, ahadi inapongojea,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Ninazivuta hatua, haraka sijatumia,
Subira kwangu ni dawa, siwachi kuitumia,
Nililokwishaandikiwa, haliwezi kuibiwa,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Wachoyo nawaridhia, choyo kukishangilia,
Laiti wangelijua, njia wanichanyatia,
Hata huko wangetua, mipaka kwenda  kutia,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Nazisogeza hatua, kule ninakoelekea,
Upuuzi kuukata, mbele ninaangalia,
Siwezi nyuma rejea, kwenye  baa na udhia,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Nimekwishatangulia, wengine watafatia,
Hapo nitapofikia, wao wataendelea,
Uhuru uliobakia, wao wakamalizia,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

Siachi kuwaombea, safari kurahisishiwa,
Zisije zuka balaa, kazi kuwaharibia,
Ila heri zikajaa, mwa kushoto na kulia,
Hapa ninapoishia, wengine wataanzia!

No comments: