Sunday, December 2, 2012

TUNAIKARIBISHA TAO



Waarabu kuungana, na ndugu Watanzania,
Neno hapo mmenena, waungwana wasikia,
Ushirikiano kufana, mema tukajichumia,
Twaikaribisha TAO, iwe na heri na nuru

Tulilingojea sana, kuja sasa kutokea,
Kwalo tukiangaliana, mikwara iliyokuwa,
Tukajichungua sana, ubaya kutokuujua,
Twaikaribisha TAO, iwe na heri na nuru!

Umeanza uungwana, kwa nafasi kutuachia,
Yetu yaweze lingana, bila ya kutuhumiwa,
Inda na zao hiyana, kidogo zikatulia,
Twaikaribisha TAO, iwe na heri na nuru!

Twaitafuta bayana, yawezayo kutufaa,
Imani kwanza kunena, mbele ikatangulia,
Kisha yakaandamana, ya tumbo kuangalia,
Twaikaribisha TAO, iwe na heri na nuru!

Wazee nao vijana, hili kulipalilia,
Miaka si mbali sana, mifano tukajaliwa,
Ionekane utwana, vingine kufikiria,
Twaikaribisha TAO, iwe na heri na nuru!

Mabidi kwa wasichana, hili litawanyanyua,
Aliamua Rabana, kitabu kukitumia,
Yazuke yenye maana, katika hii dunia,
Twaikaribisha TAO, iwe na heri na nuru!

Na mizaha kuachana, na ufisadi kutokuwa,
Hili kwsetu twaliona, budi kulipigania,
Tumeibeba amana, vingine haitakuwa,
Twaikaribisha TAO, iwe na heri na nuru!

Budi tukahimizana, kwa Mola tutarejea,
Tukipoteza dhamana, tutakuja ijutia,
Budi kulinganiana, kwa kuihofu dunia,
Twaikaribisha TAO, iwe na heri na nuru!

Nawaombea Rabana, mujarabu yote kuwa,
Kwa madogo kujafana, na makubwa nayo pia,
Daima tukapendana, na watu kusaidia,
Twaikaribisha TAO, iwe na heri na nuru!

No comments: