Monday, December 24, 2012

NIMEISHAWASIKIA



Kelele wazifungua, kama vile wazomea,

Ila nikiwasikia, vilio wanaangua,

Uchuro nautambua, si busara kuzitoa,

Nimeishawasikia, hakuna cha kuambiwa!

 

Ni mengi wamenuia, wakati ni mbovu saa,

Watu sasa wasinzia, kwa uchovu na njaa,

Yawashinda mazoea, ya zaman i wakataa,

Nimeishawasikia, hakuna cha kuambiwa!

 

Huwaona watembea, usingizini wakiwa,

Misukule hudhania, au roboti wakawa,

Kila ukiwashtua, hawachi kuongea,

Nimeishawasikia, hakuna cha kuambiwa!

 

Ndio ninaowasikia, walala wakiongea,

Maruerue yakawa, sinacho cha kuelewa,

Kikabila wakitia, sina ninalotamba,

Nimeishawasikia, hakuna cha kuambiwa!

 

Mashairi wayatia, tanzu nisizozijua,

Waghani kama ruia, na midundo ya kinaya,

Ukweli nausikia, ila sio kuelewa,

Nimeishawasikia, hakuna cha kuambiwa!

 

Ni mashaka yamekua, maneno wakiongea,

Uchimvi nauhofia, kijijini waingia,

Wana wakiangalia, wepesi kuwastua,

Nimeishawasikia, hakuna cha kuambiwa!

 

Ndoto hujiotea, jinamizi zimejaa,

Njiti awakimbilia, na vijiti kainua,

Maji nayo yafatia, moto ukifukuzia,

Nimeishawasikia, hakuna cha kuambiwa!

 

Maneno nayasikia, ujumbe sijaujuza,

Kama lugha ngeni yawa, ninashindwa kuelewa,

Au mimi nimelewa, ilhali sijajua ?

Nimeishawasikia, hakuna cha kuambiwa!

 

 

No comments: