Tuesday, December 11, 2012

Ufukara


Umasikini kuutoa, wapi wataambulia?
Hao wamenigutua, Ujerumani kujua,
Mtaji wautumia, riziki kujipatia,
Ufukara ni mtaji, wahodhi kutajirika!

Mtaji wautumia, riziki kujipatia,
Imani waikataa, pochi kwenda funguliwa,
Unasara kujitia, waongoza Tanzania?
Ufukara ni mtaji, wahodhi kutajirika!

Safari ukifatia, mengi sana zimezaa,
Utwana tuliofikia, ya kwetu kukataa,
Na msingi kuiua, amani uliyoilea.
Ufukara ni mtaji, wahodhi kutajirika!

Maskini kando kakaa, mlaji ajinasua,
Maofisa wanapaa, vijiji vinazagaa,
Wala wasio na njaa, wenye njaa wajifia,
Ufukara ni mtaji, wahodhi kutajirika!

Ni mradi umekua, wenetu unawafaa,
Kwanza wajitafunia, kisha watazicheua,
Kama kichaga ikawa, mwana tapishi apewa,
Ufukara ni mtaji, wahodhi kutajirika!

Juu walikokalia, nani atawazuia,
Ufundi sasa kugawa, na wala si kwendelea,
Na taji kujisifia, hata uongo ikiwa,
Ufukara ni mtaji, wahodhi kutajirika!

Ni lazima kuchukiwa, ubaya nikazuliwa,
Uongo nakataa, mwenyewe najionea,
Sisemi la kuambiwa, nasema la kujionea,
Ufukara ni mtaji, wahodhi kutajirika!

Mficha uchi kuzaa,  kazi ngumu itakuwa,
Mwalimu aliongea, ya maradhi kufukiwa,
Kilio huja umbua, ndilo nnalotarajia,
Ufukara ni mtaji, wahodhi kutajirika!

No comments: