Saturday, December 29, 2012

MCHAGUA SANA


 

Kuna muda na wasaa, na kitambo kupitia,

Majira usipojua, dakika zitapotea,

Ukija kuhesabiwa, masaa yemetimia,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Dahari hatukupewa, ni sekunde twaachiwa,

KIla zinapochepua, ngozi zetu zikavia,

Na pumzi huchelewa, mengi tukajichokea,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Bahati ikiwajia, bado wataichambua,

Kisha hujiinukia, mbele ikaendelea,

Halafu huangukia, pua zao kuumia,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Wa msimu huingia, upepo wa kulowea,

UKiisha wapepea, heri wakategemea,

Ukiwawageukia, kama ukichaa huwa,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Wastani huachia, zaidi kukimbilia,

Huko akishaingia, nakisi huigundua,

Nyuma akigeukia, tayari kimetwaliwa,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Uzuri atachagua, akakuta walemaa,

Rijali akivizia, akakuta una waa,

Na mme mke huwa, katika hii dunia,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Akili akifatia, huingia ukichaa,

Bora alichochagua, kikawa kinamchachia,

Werevu akaezua,  mvi akajipambia,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Mali hukimbilia, uzani ukatitia,

Mbio hapo husanzua, kwingine kuelekea,

Hali akatarajia, atakuta iko sawa,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Huko akafumania, nayo yamejichachia,

Katikati hubakia, kama amenatishiwa,

Akiweza kujitoa, nusura huwa kulia,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Kikaango hukimbia, motoni akaingia,

Huruma hatoijua, hadi majivu akawa,

Huo mwisho wake kuwa, akaiga dunia,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Ndivyo ilivyo dunia, ya mchezo na sanaa,

Saburi inaijua, kisha mkubwa wasaa,

Haraka haijaijua, ila inapojifungua,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Hchounachojionea, lenga hapo na kutua,

Kibakaika radhia, hatua utapotea,

Mwanangu binti kukaya, huu ni wangu wasia,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

Sijisumbue na kung'aa, huja kuwa ni balaa,

Mtake wako Jalia, ombilo kukuridhia,

Ibada mkiijua, yeye atawaangalia,

Kila mchagua sana, hubaki kuhangaika !

 

No comments: