Tuesday, December 11, 2012

Nyie katengezeni



Kaoneni mitaani, pamwe nako vijijini,
Hali mtaibaini, yatia shaka moyoni,
Na viongozi wa chini, sasa wakawa kazini,
Kazi yao kuharibu, nyie katengezeni!

Waliingia vyamani, ushirika kuzaini,
Uoza kutia ndani, sasa hali taabani,
VIcoba vina thamani, ushirika kuhaini,
Kazi yao kuharibu, nyie katengezeni!

Walijaa vijijini, eti kuvipa thamani,
Sanaa wakabaini, isiyo sura machoni,
Hayakuwa na auni, vijiji ni mashakani,
Kazi yao kuharibu, nyie katengezeni!

Walitinga vikaoni, halmashauri kuwini,
Leo wachakachuani, hata wasio na fani,
Miji tena sio mijini, tunarudi vijijini,
Kazi yao kuharibu, nyie katengezeni!

Waliingia benkini, hazina ni shaurini,
Vya umma kuwa hisani, fisadi wakawawini,
Leo haziko nchini, Uswizi ni maskani,
Kazi yao kuharibu, nyie katengezeni!

Walikuja michezoni, kuzikwangua thumuni,
Michango tukabaini, wakatia mfukoni,
Naona kama uhuni, chetu kuwa mkononi?
Kazi yao kuharibu, nyie katengezeni!

Kwa uongo waamini, wajiongeza thamani,
Kumbe mkubwa uduni, wananchi kutoamini,
Kukavu kwao moyoni, nani wa kumuamini?
Kazi yao kuharibu, nyie katengezeni!

Sifa gani tuwapeni, ila za umumiani,
Waongoza duniani, kwa tabia na imani,
Nani atawaamini, ila wafu kijiweni,
Kazi yao kuharibu, nyie katengezeni!

No comments: