Tuesday, December 11, 2012

Siasa za 'piga rangi



ZA rangi kwenda pakaa, ili kuwa kama mpya,
Ndiko walikofikia, na papo watabakia,
Yachemka Tanzania, kahawa inakolea,
Siasa za 'piga rangi, budi kujawaumbua!

Yachemka Tanzania, majani wanayatia,
Chai kutochakachua, asili kujipatia,
Kisha hiyo kujinywea, vitafunwa kubakia,
Siasa za tia 'pambo, uoza huuchimbua!

Urembo sasa karaha, na mapambo ni udhia,
Dhihaka wazifumua, kuwasonya wenye njaa,
Washindwa kuvumilia, kilio wanakiangua,

Wajanja waliokuwa, njia wameigundua,
Tivii zashangilia, uongo ukarembua,
Hung'ara lisilongaa, rangi za uongo kitia,
Siasa za 'piga rangi, budi kujawaumbua!

Siasa zawaishia, mapambo wakimbilia,
Ukikoga wenye njaa, bwana utawavutia,
Yako wakaangalia, na sahau kuijua,
Siasa za tia 'pambo, uoza huuchimbua!

Vitu dukani vyajaa, wachache wakununua,
Mifuko mitupu ridhaa, mbio zinazokimbiwa,
Fakiri wajiumbua, wanabaki na tamaa,
Siasa za 'piga rangi, budi kujawaumbua!

Sherehe waziandaa, bilioni kutumia,
Hali njaa yazagaa, mitaani kutembea,
Utapiamlo wajaa, kama zama warejea ?
Siasa za tia 'pambo, uoza huuchimbua!

Ya msingi kusifiwa, ili chati wakapewa,
Kumbe dhihaka ikawa, mishahara wanapewa,
Hizo kazi kutambua, ndizo walizoajiriwa,
Siasa za 'piga rangi, budi kujawaumbua!

Nini wanatuambia, hadi jipya likawa,
Barabara tunajua, kujenga wanatakiwa,
Madaraja nayo pia, na vivuko kutimia,
Siasa za tia 'pambo, uoza huuchimbua!

Maji wote tunajua, ni msingi wa familia,
Kila pande yatakiwa, wala sera haijawa,
Vipi mwajisasambua, kwalo hili kusifiwa?
Siasa za 'piga rangi, budi kujawaumbua!

Urani wanaotetea, jambo moja nawambia,
Wakajenge na kukaa, huko itapochimbuliwa,
Wana, ndugu na jamaa, pia huko kuhamia,
Siasa za tia 'pambo, uoza huuchimbua!

Wana, ndugu na jamaa, pia huko kuhamia,
Madini wakachezea, na majiye kuogea,
Miaka ikitimia, na sisi tutaridhia,
Hili wakilikataa, na nye ni kulikataa,
Siasa za tia 'pambo, uoza huuchimbua!

Sifa nyingi ni kinyaa, za ukweli hazijawa,
Vipi mtu kumsifia, kwa kaziye  kutimia,
Hili lake Tanzania, wajinga kuwazuzua ?
Siasa za 'piga rangi, budi kujawaumbua!

Mimi ninavyojua, la ajabu latakiwa,
Au huruma kutia, watu ukawaokoa,
Au walaji kukataa, chakula wakawaachia,
Siasa za tia 'pambo, uoza huuchimbua!


No comments: