Monday, December 10, 2012

Jaji kajiinamia



ABASA niliwazia, wajihi kuubetua,
Kwaye ninayemjua, kheri kuipuuzia,
Angekuwa kalatia, wala 'singejisumbua,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Nabii kakunja pua, na uso ukashupaa,
Kipofu alipomjia, na kuitaka nasaha,
Majoho waliovaa, kwanza wakapokelewa,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Wahyi kakimbiziwa, Jibrili alopewa,
Neno alipolijua, Rasuli akaugua,
Mola akamlilia, tawaba kuitikia,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Ukuu wanaopewa, dhaifu huwachukia,
Abasa kutokujua, kisa wakakielewa,
Hili sana lachangia, viumbe tukapotea,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Katika hii dunia, wana wangu nawambia,
Ami wa kukumbatia, mafukara watakiwa,
Lao lako likikuwa, mbali mtapafikia,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Nikahisi kitumbua, ukubwa  kaongezewa,
Akilini ajijua, ni muhimu amekua,
Wote tunamtambua, ombaomba tutakua,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Ukubwa nihahofia, kama pombe umekua,
Tayari ameshalewa, jinsi anavyojisikia,
Simu kaishiklia, amri azifyatua,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Nilijali historia, ukuu sikwangalia,
Mbali tulikotokea, zama jamala kapewa,
Heri nikaangalia, sipo inakotokea,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Katika hii dunia, huwa na mbili tabia,
Rehema wanaopokea, halafu wakazigawa,
Ukubwa huukataa, udhaifu  wakalea,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Kisha kunao raia, mbawa wanaojaliwa,
Hao juu watapaa,  na tai kujidhania,
Mabega yakawapwaya, kwa kutamani

mabawa,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Chini nikiangalia, thamani sijaijua,
Ndimo nitapoingia, kwa muda nisiojua,
Imani yanilemea, na wala sijawa mtawa,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

Natamni kumwambia, intaneti kufungua,
Wavuti kwenda ingia, kulo Aya za Mtawa,
Hapo akajisomea, na kuijua dunia,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

TAO ninamuombea, aipate manufaa,
Pengine haitatokea, sura tena kuijua,
Ila hilo bora kuwa, akalegeza tabia,
Jaji kajiinamia, hukumu afikiria?

No comments: