Tuesday, December 11, 2012

Hao wanaokutuma

Laiti ungelijua, ya kwamba wao watwana,
Kutumwa isingekuwa, kutma ni muamana,
Hadhi ungeinyanyua, na wao kutolingana,
Hao wanaokutuma, ubora wako hawana!

Hila wameitumia, hapo walipokubana,
Yako wakayachukua, wasio na uungwana,
Kisha wakajichagua, eti wao  ni mabwana,
Hao wanaokutuma, ubora wako hawana!

Hilo watashikilia, hadi mtakapoona,
Ila mkainyofoa, na kuihodhi dhamana,
kazi mkawaachia, kwa upya mkipatana,
Hao wanaokutuma, ubora wako hawana!

Hilo wakiligundua, itajaondoka laana,
Ya wizi ulokuwa, waziwazi twafanziana,
Mola akatujalia, kutawala kiungwana,
Hao wanaokutuma, ubora wako hawana!

Hadhi tutaifikia, ya uongozi bayana,
Ujanja isiyokuwa, ila wajua amana,
Uwakilishi ukawa, sio wa kuchumiana,
Hao wanaokutuma, ubora wako hawana!

Ubunge tukaung'oa, wenye inda na hiana,
Watu wema kujalia, hali kupiganiana,
Na sio wa kutumiwa, chinichini kupeana,
Hao wanaokutuma, ubora wako hawana!

Uwazi tutajaliwa, mambo yakaongozana,
Yote waliyoyafukia, yawe yachimbukana,
Ukweli tukaujua, pasina ya danadana,
Hao wanaokutuma, ubora wako hawana!

No comments: