Tuesday, December 11, 2012

2 0 1 3

Shule tunaingojea, kale iliyoahidiwa,
Utufunze tusiojua, kwa vitendo si ruia,
Maneno yakapwelea, upepo kuyachukua,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Kisa cha kujisifia, vya msingi vilokuwa,
Ambayo ingelikuwa, wajibu kuangaliwa,
Kama hiyo si hadaa, ndio nini kutuambia?
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Mishahara kichukua, kitu gani walipiwa,
Kama si kutujengea, barabara safi kuwa?
Na bandari  kunolewa, kazi ikajifanzia?
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Vipi mtajisifia, na mishahara mwapewa,
Kazi mlizopangiwa, wala haziojatimia,
Maji tuanyangojea, wapi mlipofikia?
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Vipi mtajsifia, hospitali zafulia,
Dawa mwachanganyikiwa, hadi feki kununua?
Udhibiti mwaogea, nini mnaangalia?
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Simu mlijiuzia, nini mnajisifia ?
Majengo mkachukua, mali yenu nayo kwa,
Viwanda vinaugua, bei mliyojipangia,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Vijiji mmeachia, maruhani kwangalia,
Na mizimu wanalia, kizazi kinavyoumia,
Imechoka nadharia, mwaenda msikojua,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Mwaenda msikojua, ya msingi nunu kuwa ?
Wajibu ukitimia, hivi utajisifia,
Kazi ya kukusudiwa, hadhi gani utapewa?
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Ona Kusini Korea,  kama pacha tulokuwa,
Ghafla wamejizoa, juujuu watembea,
Kadhalika Malaysia, angani wanakimbia.
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Mwailoga Tanzania, kudhani twaendelea,
Na matumbo yapwelea, njaa yazidi zagaa,
Utajiri wa ruia, nani humsaidia,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Fisadi wamejilia, matumboni vyakabakia,
Mezani wamefagia, hadi mabaki kutoa,
Walia Watanzania, jehanamu wahofia,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Kumi na tatu ikitua, bado nyuma yaja njaa,
Na hadithi wazitoa, eti wameshajiandaa,
Nani amekuambia, kaione historia,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Yatulemaza tabia, serikali kudhania,
Eti fadhila yatoa, pasi nayo tutavia,
Hilo ninalikataa, wamezua la kuzua,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Wala chama hakijawa, badi letu kwendelea,
Mubdi akimua, kingine chaweza kuwa,
Nadhiri mkiitia, ubaya huondolewa,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Yao wanaojivunia, wenyewe hujifanzia,
Serikali motokaa, salama kusafiria,
Na vyama twatembelea, ni viatu tunavaa,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Yatakiwa nadharia, sasa kuzungumziwa,
Maendeleo raia, ndio wanaoyazua,
Serikali mwajiriwa, kuwajibika ridhaa,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Kazi isipotimia, budi ngazi kuachia,
Mipango wanatakiwa, yote kuiangalia,
Ukweli usipokuwa, hiyo budi kuondoa,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Hesabu zinatakiwa, nini wamejifanzia,
Hadhi yaliyojaliwa, si yale ya kupangiwa,
Ikiwa yapo mapya, yafaa kuzawadiwa,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Pasina kuwa mapya, kitu gani wasifiwa,
Mishahara weshachukua, na rushwa kuzitumbua,
Ya msingi ni udhia, mtu kutaka sifiwa,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Yapo ya kujisifia, watu ukiwasauidia,
Kama vile kutokea, maji wameshajichimbia,
Bomba ukawaletea, watu wote kufikia,
Elfu mbili ukifika, halafu kumi na tatu:
Sote tupeleke shule, wakubwa wa Tanzania!

Ukweli wa kuendelea, ni watu kujifanzia,
Ya kwao kusaidiwa, ili yapete kutimia,
Maendeleo huvia, mtu anapotafutiwa,

No comments: