Tuesday, December 11, 2012

Hujui !



AHADI haujapewa, ivute nyuma hatua,
Mbele ukijipangia, inshalla kufatia,
Kiburi ukijitia, inakusoma dunia
Asubuhi ukiamka, je, jioni utafika?

Usiku ukiingia, usiache omba dua,
Mshukuru na Jalia, nusu kifo hujapewa,
Siku hautoijua, kuamka kutokuwa,
Usiku unapolala, asubuhi utafika?

Kitabuni kakwambia, kusudi la kuzaliwa,
Yeye kumtumikia, vingine vikafatia,
Jeuri ukiitia, yeye akuangalia,
Asubuhi ukiamka, je, jioni utafika?

Bismika yatakiwa, allahuma kuitia,
Na amutu ahaiya, ndivyo inavyotakiwa,
Ni maiti utakuwa, omba kesho hai kuwa,
Usiku unapolala, asubuhi utafika?

Allahamdu kutoa, mema utazawadiwa,
Kiumbe haukujua, utaona tena jua,
Muhimu kushangilia, kwa bwana kumsifia,
Asubuhi ukiamka, je, jioni utafika?

Ujibari ni balaa, inachukia dunia,
Ardhi huwa yalia, iombe ndani kutiwa,
Ikakubane kifua, kwa niaba ya radhiya,
Usiku unapolala, asubuhi utafika?

Kesho yangu sijajua, Manani namuachia,
Riziki kuangalia, na hifadhi kuijua,
Zaidi nimekataa, katiti kukumbatia,
Asubuhi ukiamka, je, jioni utafika?

Naitazama dunia, mizigo ikipakua,
Kudumu ilodhaniwa, nayo inajiozea,
Waondoka mashujaa, dahari waliolea,
Usiku unapolala, asubuhi utafika?

Wale wanaomzulia, bila ya kujiseomea,
Jambo wakalielewa, na uongo kukataa,
Wakabaki kujutia, elimu walifulia,
Asubuhi ukiamka, je, jioni utafika?

Viranja wanaojua, watubu nyuma ya pazia,
Kosa lake historia, sasa wanasingizia,
Ila wale wasiojua, lusifa awahadaa,
Usiku unapolala, asubuhi utafika?

Ushahidi wapwelea, bado wanang'ang'ania,
Shadidi nari ikawa, sasa inawangojea,
Dhikirini  manufaa, watu wakajiokoa,
Asubuhi ukiamka, je, jioni utafika?

Aliamin radha, uzidi kutuomboa,
Kulia ulikokaa, nusura twaililia,
Na wewe mchaguliwa, lako hutokataliwa,
Usiku unapolala, asubuhi utafika?

No comments: