Tuesday, December 11, 2012

Sura nzuri ukikosa

Sura usipojaliwa, umbo kamili kamia,
Asili lililokuwa, si ya mchina kutwaa,
Hayo yatakuumbua, pini huwa zapasua,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!

Uzuri ukifulia, usikose na tabia,
Hapo utapungukiwa, dunia ukaichukia,
Wapo wasiojaliwa, wanashinda kwa tabia,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!

Uaminifu ogea, posa haitachelewa,
Ni sabuni ya kufaa, sura mbaya hupungua,
Heshima ukikamia, wapo wanaofurahia,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!

Uongo ukikataa, na ukweli kuitetea,
Watu utawazuzua, uzuri ukageewa,
Ukija kushtukia, tiviini unang'aa,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!

Watu watakupotea, mwingine kukudhania,
Lulu ukaigundua, uzee unaingia,
Kiumbe kinyonga huwa, sura akageuzia,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!

Mahaba ukiyajua, waume huwanyanyua,
Sura kutofikiria, mengine kuangalia,
Watu wakawashangaa, tofauti mlivyokuwa,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!

Hupendwa wa sura mbaya, naa mzuri aliyekuwa,
Sababu ninayojua, mshale una shabaha,
Vingine haitakuwa, ila huruma ikawa,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!

Akili ukijaliwa, sura mbaya hufifia,
Kifaru unapokuwa, uzuri utajaliwa,
Watu wanaangalia, wapi utapafikia,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!

Usomi ukinukia, mabinti utawazoa,
Nje wanatarajia, lazima utawachukua,
Wana mkenda kuzaa, akili wasiovua,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!

Hayo ni yake dunia, hapa mimi naishia,
Nimelola na kuzua, mbali nikifikira,
Muumba ana usawa, mizaniye hutimia,
Sura nzuri ukikosa, omba umbo kujaliwa!


No comments: