Saturday, December 29, 2012

Hatuwezi kulingana



Sifa sijaitafuta, na wala sintoitaka,
Sijipakai mafuta, ngozi yangu yatakata,
Hapa kinachonileta, haki isiwe wahaka,
Hatuwezi kufanana, nyie mnataka sifa:
Mie ninataka dawa !

Majibu ninatafuta, majawabu sijashika,
Kukariri sijadata, ila fikra nazitaka,
Na uongo kuuteta, kwangu huwa ni dhihaka,
Hatuwezi kufanana, nyie mnataka sifa:
Mie ninataka dawa !

Mna ndoto za kuota, nalitaka la hakika,
Mwajijengea ukuta, ila wangu wabomoka,
Kila muweka matuta, usalama autaka,
Hatuwezi kufanana, nyie mnataka sifa:
Mie ninataka dawa !

Ya kwenu ni kupepeta, mimi ni kuhangaika,
Kazi yangu si kusuta, ila bayana kuweka,
Kama nyie chuma-leta, mimi yangu kulimika,
Hatuwezi kufanana, nyie mnataka sifa:
Mie ninataka dawa !

Ya kwenu ni ya kung'ata, vigumu kutafunika,
Meno yenu ya kukata, hali yetu yapangika,
Mkiyachota kwa kata, yetu yaja kwa birika,
Hatuwezi kufanana, nyie mnataka sifa:
Mie ninataka dawa !

Nyie mnapojiokota, sisi kwanza tunashuka,
Mikono mkipepeta, siye twaanza kuvuka,
Twaogelea ukata, nyie mmetajirika,
Hatuwezi kufanana, nyie mnataka sifa:
Mie ninataka dawa !

Mkata kaziye kusota, shoga hakubahatika,
Zama pakiwepo kota, leo ghorofa zazuka,
Kumbe maisha huchota, wengine wakamwagika?
Hatuwezi kufanana, nyie mnataka sifa:
Mie ninataka dawa !

No comments: