Monday, December 24, 2012

Kiswahili hakipendwi

Ushairi wachukiwa, kwa kuwa Uislamu,
Kafiri wauzulia, hadi waitwa haramu,
Hawataki kuulea, ikaufaa hirimu,
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Sasa wauhofia, imani kutakadamu,
Akili utazibua, wakafahamu muhimu,
Kisha wakayalilia, yaliyokuwa magumu,
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Wanaouchakachua, lengo wameliazimu,
Hadhi ipate pungua, watu wasiwe na hamu,
Ndio mana waingia, kwenye mipasho kukimu,
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Rusharoho yao njia, asili kuidhulumu,
Taarabu yenye njaa,isiyo na ubinadamu,
Karata waichezea, vya kweli kuvihasimu,
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Redioni wazuia, na kurusha yagharimu,
Chombo wameishajua, kwa wengi huwa rahimu,
Hayo watayasikia, kisha yaweze kudumu,
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Mtandao waingia, imani kuidhulumu,
Kaswida wanafumua, ukimya kuuhukumu,
Watu wasiposikiya, daawa sio karimu,
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Fani wanaichengua, tivini si adhimu,
Ni viuno kunengua, kwa masaa nazo zamu,
Matako kutingishia, kushibisha zao hamu,
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Tabia yao balaa, utu inatugharimu,
Na dini sasa nazaa, umebaki uhujumu,
Wakubwa wanunuliwa, kuujenga udhalimu,
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Yarabi twakulilia, kuangalia kaumu,
Yake yakarejeshewa, kabla ya yako hukumu,
Vingine haitakuwa, salama wala salamu,
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Wakwasi tukishakuwa, hadhi itajipandia ?
Mapeni tukishajaa, tutaweza kinunua,
Mapambo tukakitia, kwenda kuuza Russia ?
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Vyuo tukitunukiwa, vyenye sifa za kufaa,
Itake kuja dunia, na sisi kuwafunzia,
Hapo ndege itapaa, na watu kukimbilia ?
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

Mifano tunaijua, shilingi twaichezea,
Tukazidi kuchelewa, kama yangoja dunia,
Twajiona na wasaa, kumbe nyuma twarejea?
Kiswahili hakipendwi, eti ni cha masikini !

No comments: