Monday, December 24, 2012

Hakiwi unachotaka



Mja rudisha hatua, taratibu kutembea,
Dunia mwana izaya, radiki hajatokea,
Ila Alaa kuridhia, nabiya na waliiya,
Hakiwi unalotaka, bali ni liandikwalo!

Udikteta yajua, hiyo ni yake tabia,
Wazo haitangojea, kwa nani kuja tokea,
Yake ikishaamua, ndio hayo yanakuwa,
Hakiwi unalotaka, bali ni liandikwalo!

Wengi imewachezaya, walodhani waijua,
Chenga ilipowatia, golini wameshatua,
Kisha lao kutokuwa, na mengine kutokea,
Hakiwi unalotaka, bali ni liandikwalo!

Hupangwa likatimia, lilioishaandikiwa,
Kwa siku na yake saa, vingine haitakuwa,
Hakuna la kuzidia, wala linalopungua,
Hakiwi unalotaka, bali ni liandikwalo!

Mahala huchaguliwa, na mandhari kupangiwa,
Na hadhara huingia, ile ilokusudiwa,
Na habari huzijua, kazi waliopangiwa,
Hakiwi unalotaka, bali ni liandikwalo!

Wako aweza akawa, ila hautojaliwa,
Huja ukayasikia, wengine wakiongea,
Hadithi husimulia, kama usiyemjua,
Hakiwi unalotaka, bali ni liandikwalo!

Shukrani wanatoa, waomba kukubaliwa,
Yao yakawatokea, kama walivyoombea,
Ni nasibu maridhawa, na wachache hujaliwa,
Hakiwi unalotaka, bali ni liandikwalo!

Atujalie Jalia, yetu tukayang'amua,
Saa tukaitambua, na kuweza jiandaa,
Na mzoga kutokuwa, tushindwe isoma dua,
Hakiwi unalotaka, bali ni liandikwalo!

No comments: