Tuesday, December 11, 2012

Juhudi bila akili

Inakuwa ujahili, juhudi bila akili,
Mtu akafuja mali, pasi lile wala hili,
Pasiwe na afadhali, bali ni ubaradhuli,
Juhudi bila akili, mtu haufiki mbali!

Juihudi bila akili, huwa si yetu asili,
Binadamu si anzali, yeye mashine kamili,
Akichakata maswali, anaupata ukweli,
Juhudi bila akili, mtu haufiki mbali!

Mtu si kiwiliwili, bali huwa ni akili,
Hali ataikabili, mazingira na mahali,
Hakiwi kitu muhali, panapo yake adili,
Juhudi bila akili, mtu haufiki mbali!

Ukiiona dalili, juhudi bila akili,
Kajiulize maswali, nini wanachonakili,
Hadi wakawa bahili, kuzichangia akili ?
Juhudi bila akili, mtu haufiki mbali!

Ubongo wetu mithili, ya jambia la makali,
Hakuna kinachohimili, pale tunapokabili,
Ila kuna majahili, hawaupendi ukweli,
Juhudi bila akili, mtu haufiki mbali!

Ili kuna majahili, hawaupendi ukweli,
Fikira kwao muhali, ila wazipenda hali,
Ukubwa kwao ni ghali, kwa wengi si afadhali,
Juhudi bila akili, mtu haufiki mbali!

Huwa ni mbwa wakali, wakakataa kubuli,
Wakajitia muhali, kuzikabili kauli,
Wakavaa mabakuli, na mkononi bangili,
Juhudi bila akili, mtu haufiki mbali!

Kwa kuzomea ni nguli, na vigelegele mali,
Kufikiri si asili, wala haiwi fasili,
Huona ni idhilali, vichwa vyao kuhimili,
Juhudi bila akili, mtu haufiki mbali!

No comments: