Huhangaika mkiwa, na hii kubwa dunia,
Shabaha aliyepwaya, hawezi akapatia,
Kila akifikiria, pengine atatungua,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Wengi nimeshuhudia, ujanja walijitia,
Kwa kiburi kujitia, kulenga wamesomea,
Ila kilichofatia, washinda kushuhudia,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Karibu waliyaachia, mbali wakayazuikia,
Kuja kutahamakia, mkenge wameingia,
Na walilolidhania, kama kweli halikuwa,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Kwa pembeni wafulia, ukutani
kuingia,
Kulalama wabakia, pengine wamechezewa,
Au wamehujumiwa, wala haki haikuwa,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Kilio watakizua, machozi wakayatoa,
Macho yaliathiriwa, uchafu ukaingia,
Au homa kuingia, ghafla mwili kulewa,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Yote ukiangalia, mwee, wanasingizia,
Ziliwazidi tamaa, huku na huku kwingia,
Saa ilipofikia, wkadhindwa kuamua,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Ndiyo yanayotokea, kwa wengi wa Tanzania,
Kwa walilojitakia, kuwa limewakataa,
Na walilolichukia, ndio sasa lawafaa,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Wapo walioolewa, hali ni bahati mbaya,
Mme mpenzi hajawa, na mkewe aidha pia,
Wanauzusha ubia, subira na kuvumilia,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Hawezi kushangaa, DNA yachukiwa,
Kwa kuizua balaa, na kweli ikazagaa,
Walio na maridhia, mkono hawajajaa,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Bwanangu mwenye kujua, neno ninakuachia,
Siri yangu waijua, na vyangu vilivyokuwa,
Asante kwa kuridhia, haki yangu kuipewa,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
Wivu sitajionea, wenye vyao visokuwa,
Kidogo nilichopewa, kinaweza kunivua,
Subira nitailewa, pasina kulewa dunia,
Asiyejua shabaha, halengi
mpaka kufa!
No comments:
Post a Comment