Saturday, December 29, 2012

Akrabu

Mshale ningeliweza, wa saa nyuma kuweka,
Saa ningeirejeza, siku iliyotukuka,
Siku ninayoiwaza, hata baada ya miaka,
Akrabu ningeweza, kuurudisha tena nyuma!

Saa ningeifikiza, mwanzoni ikaanzia,
Ili nipate kuweza, fanza niliyoachia,
Tana nikajihimiza, ziada kuongezea,
Akrabu ningeweza, kuurudisha tena nyuma!

Yangu ningetengeza, maslahi kujaliwa,
Sio yale yenye giza, nuru yasiyoyajua,
Bali yale ya mwangaza, mwanga usikopungua,
Akrabu ningeweza, kuurudisha tena nyuma!

Mwenyewe ninajibeza, kwa kuwa nimechelewa,
Kwa kukawia kuanza, wa mwisho ninaishia,
karata nitayocheza, sijui cha kuibua,
Akrabu ningeweza, kuurudisha tena nyuma!

Nafsi niliipendeza, roho nikaibomoa,
Na leo najiuliza, wapi kwangu kupitia,
Nini nitakchoweza, msamaha nikapewa ?
Akrabu ningeweza, kuurudisha tena nyuma!

No comments: