Monday, December 10, 2012

K U T A K A



TAMAA mama wa nazaa, uroho ameumbiwa,
Kitu atakililia, kisichomsaidia,
Mpaka akaugua, na kujiona mkiwa,
UNAWEZA ukataka, lakini yakakushinda!

Kauli ataitoa, uwezo amejaliwa,
Ila anapojaliwa, kubangaiza ikawa,
Hucheza pata potea, na huku ajivunia,
UNAWEZA ukataka, lakini usiyaweze !

Hayawi ya kumfaa, ila ya kumuumbua,
Nyasi zikajiotea, mlo unapotakiwa,
Na magugu yakamea, maji yanapoliliwa,
UNAWEZA ukataka, lakini yakakushinda!

Rangi atazitumia, kujipamba kulanjia,
Ilhali kajaliwa, kujitangaza ridhaa,
Huzuka kisichokuwa, kifaacho kujifia,
UNAWEZA ukataka, lakini usiyaweze !

Kisha atakazania, kuikusanya dunia,
Dunia ikikataa, moyo utamzindua,
Muhemuko ukitua, kilema akabakia,
UNAWEZA ukataka, lakini yakakushinda!

Juu atajinyanyua, Mola chini sasa kuwa,
Jema kutoliskia, akatafuta ubaya,
Milki akailea, alompa kuchukiwa,
UNAWEZA ukataka, lakini usiyaweze !

Imani huikomoa, mtihani kuitia,
Vurugu akaachia, itaabike dunia,
Umma akaufukia, na sio kuunyanyua,
UNAWEZA ukataka, lakini yakakushinda!

Ya kwao huyaezua, mbali akayatupia,
Majengo akachimbua, yake akayandaa,
Na viwanja kunadiwa, anavholinda Jalia,
UNAWEZA ukataka, lakini usiyaweze !

Hapo wakajichimbia, haramu huvinunua,
Halali wakakataa, na ujibari kuzaliwa,
Utukufu kujitia, moto unaopalilia,
UNAWEZA ukataka, lakini yakakushinda!

Ila huishi kwa saa, hata siku haijawa,
Baragumu hujalia, chooni wajiinamia,
Au maji wayatia, tohara yasiyokuwa,
UNAWEZA ukataka, lakini usiyaweze !

Sakramuti ki'ngia, vishindo huvisikia,
Kukurukakara ikawa, hadi roho kutolewa,
Awali zaja hidaya, nusu watu kurejea,
UNAWEZA ukataka, lakini usiyaweze !

RABANA mtegemewa, yote unajionea,
Kilio wakisikia, cha waja wanaoonewa,
Haki wameinunua,  dhuluma kutugawia,
UNAWEZA ukataka, lakini usiyaweze !

No comments: