Monday, December 24, 2012

Wazee wako nje


KETE wamezipania, bao kuliandamia,
Chini ya mti wakaa, upepo kuwakumbatia,
Kisha ukawapepea, na majasho kuwatoa,
Wazee  nje wakaa, hali ndani kwaungua ?

Chao walishachukua, mapema ilivyokuwa,
Sarakasi waachia, wenye macho kwangalia,
Kelele wazisikia, furaha waidhania,
Wazee  nje wakaa, hali ndani kwaungua ?


Na walipojikalia, hawana la kujionea,
Ndani yanayotokea, yazuia mapazia,
Kilio kikianguliwa, kicheko hugeuziwa,
Wazee  nje wakaa, hali ndani kwaungua ?

Akhera wazungumzia, wala siyo ya dunia,
Wakajifanya wajua, malaika na ismia,
Majina kujitajia, wajao kuwatokea,
Wazee  nje wakaa, hali ndani kwaungua ?

Kisha wakakumbushia, enzi zao za kutuwa,
Na waliyokadiria, viumbe yatawafaa,
Misingi wakajitia, mchanga hawakutia,
Wazee  nje wakaa, hali ndani kwaungua ?

Na stima walitia, hakika iliyokuwa,
Nyumba kutokuungua, sembuse kuteketea,
Kicheko wakaangua, ujanja kujisifia,
Wazee  nje wakaa, hali ndani kwaungua ?

Harufu wakasikia, nyama choma zanukia,
Ila ziliwazidia, kwa ukakasi kujaa,
Na moshi kujibetua, hayo yakawagutua,
Wazee  nje wakaa, hali ndani kwaungua ?

Hivi nyumba yaungua, hali hapa tumekaa,
Ujinga au balaa, au tumelogewa ?
Vicheko vikajifia, na kuingia ukiwa,
Wazee  nje wakaa, hali ndani kwaungua ?

Siku hiyo naijua, mimi nimejionea,
Iko njiani yaingia, taratibu bila riha,
Mtu haitamstua, hadi litakapotokea,
Wazee  nje wakaa, hali ndani kwaungua ?


No comments: