Saturday, December 29, 2012

Pazia lafunguliwa



Lakunjuliwa pazia, tuone yanayotokea,

Mwaka unakaribia, Januari kuingia,

Nangojea potezea,  jinsi zitakavyokuwa,

Pazia lafunguliwa, la sanaa na viroja !

 

Nazingojea sanaa, zitakavyonistua,

Akili zilizolemaa, wenda zikashtuliwa,

Hali yangu kurejea, uhakika nikajua,

Pazia lafunguliwa, la aibu na fedheha !

 

Pazia la madini gawa, na hisabu kupotea,

Akili kuzilalia, mfukoni kuzitia,

Na hongo kuinunua, uwezayo kununua,

Pazia lafunguliwa, la sanaa na viroja !

 

Pazia mafuta haya, na nani ayanunua,

Na mchezo kuchezewa, uwanja usiokuwa,

Bei ikapotezewa, na uchumi kuchafua,

Pazia lafunguliwa, la aibu na fedheha !

 

Pazia umeme njaa, njiani unaoishia,

Hamsini kutimia, robo haijafikia,

Visababu kwa gunia, haviachwi kutolewa,

Pazia lafunguliwa, la sanaa na viroja !

 

Pazia la maji mwaa, watu wasiyojionea,

Na ahadi zajifia, bila ugonjwa kujua,

Kilio kutosikia, ila mazishi yakawa,

Pazia lafunguliwa, la aibu na fedheha !

 

Pazia la ng'ombe waya, na vijosho vya kwogea,

Nasaba ikanukia, na ujanja wa kijuha,

Heri inakopepewa, hadi moto kuuzua,

Pazia lafunguliwa, la aibu na fedheha !

 

Pazia la Swizi gea, na vigia vya kutia,

Waliojikusanyia, na vilango kupitia,

Uchama ukawatoa, kama wanavyoutoa,

Pazia lafunguliwa, la sanaa na viroja !

 

Pazia la kufunikia, daktari kutegewa,

Kisa haki kulilia, ubaya akazuliwa,

Mwee, ninajichukia, kama nisiyezaliwa,

Pazia lafunguliwa, la aibu na fedheha !

 

Pazia la kufukia, wala si kufundishia,

Walimu walilolivaa, na kushindwa kuwafaa,

Vitumbua kugawiwa, vya kuokewa sheria,

Pazia lafunguliwa, la sanaa na viroja !

 

Batili yaendelea, na haramu yanadiwa,

Haki wameifungua, dhuluma waifungua,

Tarakimu kutimia, maajabu nangojea,

Pazia lafunguliwa, la aibu na fedheha !

No comments: