Saturday, December 29, 2012

AMANI KAMA TUNDA

WAOVU ukiachia, mabichi wanaaangua,

Wende kuvundukia, wewe usipopajua,

Juu kwa juu ikawa, bei wanapatania,

Amani yetu ni tunda, nani anatunza shamba  ?

Miti msipoangalia, magugu hujiotea,

Ikawa shida kuzaa, mti unapohujumiwa,

Matatizo huzushiwa, hadi shamba kukimbia,

Amani yetu ni tunda, hivi mti twautunza ?

Na maji pasipokuwa, mti waweza sinyaa,

Mchwa wakafurahia, chakula chao kikawa,

Wakua ukidhania, kumbe wenda kujifia,

Amani yetu ni tunda, mti twastawishaje  ?

La bibi linapokuwa, watu wakajichumia,

Hasara mtaingia, mwizi pasi kumjua,

Haki wamejigawia, nini utaambulia ?

Amani yetu ni tunda, shamba amiliki nani ?

Miti inapochakaa, mipya huwa yatakiwa,

Mbegu usipojaliwa, hutoweza jipandia,

Vya kale vikiendelea, huja kuvuna udhia,

Amani yetu ni tunda, mbegu twazipata wapi ?

Mti wataka mbolea, pia maji kumwagia,

Hasa katika dunia, mvua ilikopotea,

Bila hivyo kikawia, waweza jinyaukia,

Amani yetu ni tunda, mti twastawishaje  ?

Jasho mwaweza kutoa, pasiwe cha kuambulia,

Sababu mia kutoa, kwanini mmefulia,

Ikawa kusingizia, tatizo kisichozua,

Amani yetu ni tunda, shamba amiliki nani ?

Sayansi inatakiwa, pia kwenda kutumia,

Sasa ni kunyunyizia, tone kwa kila hatua,

Kwayo mti ukakua, na maua kuchanua,

Amani yetu ni tunda, mbegu twazipata wapi ?

Maji katika dunia, sasa yanakopotea,

Mikakati yatakiwa, kidogo kutoshelea,

Watu wakaajabia, kuwa wasilodhania,

Amani yetu ni tunda, mti twastawishaje  ?

Yajapo yakatokea, umiliki kuvamiwa,

Na wanaoyasimamia, wao pembeni kukaa,

Wakateza na sheria, kukunja na kukunjua,

Amani yetu ni tunda, shamba amiliki nani ?

Hasira huziibua, kwa wanaofatilia,

Kuwatuliza huvia, mishipa wakatanua,

Mhemuko ukikua, huja kuzuka balaa,

Amani yetu ni tunda, mbegu twazipata wapi ?

Mti ukijaugawa, pande moja kumwagia,

Ajabu haitakuwa, nusu kufa, nusu zaa,

Bali wote utavia, na mwisho kuteketea,

Amani yetu ni tunda, mti twastawishaje  ?

Chanzo msipokijua, dalili mkaagua,

Huja kushtuliwa, maradhi yakizidia,

Hujivunga wakujua, kupata pa kupenyea,

Amani yetu ni tunda, shamba amiliki nani ?

Mbegu wakizifukua, wakaanza kujilia,

Pasiwe kurudishia, uhai kuendelea,

Watajazuka vichaa,  mapanga yakatembea,

Amani yetu ni tunda, mbegu twazipata wapi ?

Wanaoiba mbolea, na vipando kuvitwaa,

Vyao wakajifanyia, kwanza wanakimbilia,

Wengine wakafulia, huja wakaambuliwa,

Amani yetu ni tunda, mti twastawishaje  ?

Juu waliokalia, budi macho kufungua,

Kwa sawa kuangalia, hali hasa wakajua,

Vingine ni kutania, na kuchezea dunia,

Amani yetu ni tunda, shamba amiliki nani ?

Nani anatuhadaa, mti tunaufatia,

Kisha tukajipandia,  huko tusikoruhusiwa,

Tunga linaning'inia, twataka kujichumia ?

Amani yetu ni tunda, shamba amiliki nani ?

Kila nikiangalia, haki na usawa bandia,

Mwivi namgundua, ndiye ananyemelea,

Macho tunawafumbia, vingine kusingizia,

Amani yetu ni tunda, shamba amiliki nani ?

No comments: