Tuesday, December 11, 2012

Jobless

WAJUMBE wameingia, ajira wasiokuwa,
Kila mtu ajitia, mkulima amekuwa,
Au anajitolea, chama kukitumikia,
Joblesi waliokuwa, viongozi wachagua ?

Hali ilivyofikia, mashaka inanitia,
Kazi wasioijua, nani watamchagua,
Haitawaponza njaa, mtoa riziki kupewa?
Joblesi waliokuwa, viongozi wachagua ?

Njaa ya demokrasia, yatupeleka pabaya,
Uoza kuuchagua, nchi ukasimamia,
Zuio sijalijua, labda katiba mpya,
Joblesi waliokuwa, viongozi wachagua ?

Maamuzi ni sanaa, usomi unatakiwa,
Mambo ukayajua, kwa akili kutumia,
Si moyo kuutumia, kwa huruma kuwazia,
Joblesi waliokuwa, viongozi wachagua ?

Wajumbe wanatakiwa, misingi kuitambua,
Ipo demokrasia, yatakiwa heshimiwa,
Kazi sio kuzomea, au kuishangilia,
Joblesi waliokuwa, viongozi wachagua ?

Tofauti wasiojua, kweli -uongo ikawa,
Nini watatusaidia, ila tu kununuliwa,
Ni mafuu twachukua, ugonjwa kwenda ulea,
Joblesi waliokuwa, viongozi wachagua ?

Siasani ni balaa, ujinga mkiulea,
Wenyewe utawaambua, Amin akitokea,
Mjanja aliyekuwa, na kiti kupigania,
Joblesi waliokuwa, viongozi wachagua ?

Ya Uganda kuyazua, hapa kwetu Tanzania,
Kisa ujinga kulea, vyamani ukazagaa,
Kwa wongo kushangilia, na kweli kuizomea,
Joblesi waliokuwa, viongozi wachagua ?

No comments: