Monday, December 10, 2012

Shamba la bibi lachoka

RUTUBA tena halina, wamekwishalikwatua,
Mazazi lina hiana, hakuna kinachokua,
Wasafisha waungwana, watu wanaochagua,
Shamba la bibi lachoka, wapi kweingine waende?

Hayakuanza kwa jana, miaka inafikia,
Ilikuwa muamana, cha umma kukikwangua,
Hapa tulipofikishana, sasa ndiyo twayajua,
Shamba la bibi lachoka, wapi kweingine waende?

Wanaumia watwana, kwa uniti kupakaziwa,
Kipato tunagawana, wana njaa wakalia,
Walio juu hiana, hadithi wasimulia,
Shamba la bibi lachoka, wapi kweingine waende?

Mikataba ya kuchuna, mingi walishaingia,
La swalaa na adhana, hakuna aliyesikia,
Chama waliongozana, na wao wakitumia,
Shamba la bibi lachoka, wapi kweingine waende?

Yajulikana bayana, watu wajinyamazia,
Ni nai wa kulingana, uweze mlingania,
Wao sasa ni mabwana, kila kitu wanajua,
Shamba la bibi lachoka, wapi kweingine waende?

Ya  muongo ni fupi sana, ni nani asiyejua,
Yataangziwa mchana, nasi sote kuyajua,
Walio wajanja sana, wajinga sana wakawa,
Shamba la bibi lachoka, wapi kweingine waende?

No comments: