Saturday, December 29, 2012

Mpenda vya ukoloni




Sheria za jalalani, zisibaki vitabuni,
Uhuru tulishawini, twafhifadhi ukoloni ?
Nani ataliami, atokaye Ulayani ?
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Kama hapana uhuni, basi sisi majinuni,
Au tunayo moyoni, haki yasiyoamini,
Raia twawazaini, hali nasi wakoloni ?
Muenzi vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Misingi hatuamini, usawa inayowini,
Tunaufanya utani, ustawi kuzaini,
Huu sio uhaini, ukiwemo katibani ?
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Viongozi duniani, raia wanazaini,
Watwaa ya ukoloni, kuhodhi madarakani,
KIlichokuwa uhuni, sasa chapewa thamani,
Muenzi vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Kuna mabomu yakini, ya machozi na hewani,
Hayachagui ni nani, atupiwa uwanjani,
Wazee na afkani, wote watiwa kundini,
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Sheria za uhaini, zawaficha watu ndani,
Dhamana ikawa guni, japo iko katibani,
Ya mtu wayathamini, sio yalo sheriani,
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Mikutano na maoni, yakatolewa uzani,
Wakaingia vitani, kodi inayoauni,
Mlipa akawa duni, kama damu na mumiani,
Muenzi vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Kuna nyingi za kihuni, waziachia nchini,
Haki haziithamini, ila kulinda fulani,
Zisizotiwa ubani, wala usawa kuwini,
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Uhuru wetu ni chini, viwango haujawini,
Katiba zungumzeni, uhuru kuuthamini,
Kisha kutathmini, chapungua kitu gani,
Muenzi vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

No comments: