Saturday, December 29, 2012

Toka lini mshirikina

Mshirikina amini, amekuwa ni kuhani,
Kaingia hekaluni, joho li  kisiginoni,
Ameremeta yakini, kama taa ya imani,
Toka lini mshirikina, akawa ni mcha mungu ?

Molawe yuko nyumbani, kabakia kabatini,
Kamchonga kwa makini, ndiye humpa imani,
Akienda hekaluni, huwa ni uchi mwilini,
Toka lini mshirikina, akawa ni mcha mungu ?

Ibada yake shetani, kamjengea moyoni,
Majini wamdhamini, na maruhani kuwini,
Na mikoye ni ghalani, kaihifadhi darini,
Toka lini mshirikina, akawa ni mcha mungu ?

Akiranda mtaani, mitumewe mfukoni,
Hao anawaamini, humlinda majiani,
Kwa talasimu kifani, shingoni na kiunoni,
Toka lini mshirikina, akawa ni mcha mungu ?

Atadamka manani, kumsikiza shetani,
Kisha akatathmini, muda wa kuwa kundini,
Mkaona ibadani, naye yumo miongoni,
Toka lini mshirikina, akawa ni mcha mungu ?

Asubuhi na jioni, kutabana ni hisani,
Kaitwa majaribuni, na vibwete vya majini,
Hakosi mkutanoni, kuyapata madhumuni,
Toka lini mshirikina, akawa ni mcha mungu ?

Mizimu ataamini, kuliko wana nyumbani,
Shari wakishaazini, asipotii haini,
Kuua yake husuni, na ngome ushirikinani,
Toka lini mshirikina, akawa ni mcha mungu ?

Kapewa akili dunia, ahera na duniani,
Jema hatolibaini, ila akirizaini,
Akaijenga imani, ahame toka uthani,
Toka lini mshirikina, akawa ni mcha mungu ?

No comments: