Saturday, December 29, 2012

MMILIKI WA KATIBA NANI ?

 
 
KATIBA naiusia, mmiliki kutajiwa,
Tupate kumtambua, watu wote Tanzania,
Asije akatokea, tapeli kutuzingua,
Mmiliki wa katiba, lazima atambuliwe!
 
Ninavyojua raia, mmiliki atakuwa,
Pawa zote akapewa, kuamua, kutengua,
Kura akiitumia, au njia ya kufaa,
Mkubwa wa serikali, lazima tumtambue !
 
Afrika watibua, katiba kuzichezea,
Watumishi kuchukua, na haki wasichokuwa,
Ukuu kujipalia, mkaa usiokuwa,
Mkubwa wa kila kitu, lazima ajulikane!
 
Kisha kung'ang'ania, pale wasipotakiwa,
Ni vigumu kuachia, madhambi tukayajua,
Wanapenda kujifia, ikulu wanakokaa,
Mmiliki wa katiba, lazima atambuliwe!
 
Muundo unatakiwa, hili likaamuliwa,
Nami ninawausia, mabunge yanatufaa,
Juu yakishakua, na uchama kujifia,
Mkubwa wa serikali, lazima tumtambue !
 
Mawili yanatakiwa, taifa  kutumikia,
La kawaida likawa, la wanaochaguliwa,
La upili kuzaliwa, kwa fani na tasnia,
Mkubwa wa kila kitu, lazima ajulikane!
 
Hisabu ikatimia, kwa makundi kuingia,
Watu yakiwatetea, na wapweke kutokuwa,
Haya yatapokuwa, hukaa juu raia,
Mmiliki wa katiba, lazima atambuliwe!
 
Nadiriki kuongea, kuhusu pia  mikoa,
Mkuu anatakiwa, naye akachaguliwa,
Kisha akasaidiwa, na bunge la wake mkoa,
Mkubwa wa serikali, lazima tumtambue !
 
Thelathini yatakuwa, Mtwara ndani ikiwa,
Haki zao kutetea, kama gesi kuwafaa,
Katu wasingechezewa, kama wanayotezewa,
Mkubwa wa kila kitu, lazima ajulikane!

No comments: