Tuesday, December 11, 2012

Ishi nao matajiri

USIA nakuachia, binti yangu maridhia,
Mtego kuukimbia, huruma ukajaliwa,
Masikini si udhia, kwako wewe yako njia,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Kwako wewe yako njia, peponi kwenda ingia,
Ikutahamini dunia, na kukuona shujaa,
Hawa ukitumikia, asante yao hukaa,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Matajiri nao kaa, yao utayasikia,
Wengi wao washupaa, hazina kutegemea,
Uungu wakajitia, kesho kutoangalia,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Enenda wasaidia, ujira ukautwaa,
Ila ya kwao tabia, kwako haitakufaa,
Mabega kutonyanyua,l na kuifinyiza pua,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Mabega kutonyanyua, na kuifinyiza pia,
kwa kuwaona udhia, watu wasiojaliwa,
La kwao lako likiwa, mbali huendafikia,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Maradhi hayajakuwa, ufakiri watibiwa,
Akili ukifungua, njia zake utajua,
Wasajaishe raia, hilo wataliondoa,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Msingi ukijiengea, nyumba watainyanyua,
Na nguzo wakazitia, hadi ghorofa ikawa,
Subira ukiilea, haya utafurahia,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Mamlaka walopewa, mtaji wautumia,
Etik kwao wahofia, ufakiri kuundoa,
Kesho wanaidhania, watakuja wakataa,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Umaskin waulea, kutawala kwendelea,
Ombaomba wakijaa, sadaka watafatia,
Nafuu ukiachia, waweza jitegemea,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Nafuu ukiachia, waweza jitegemea,
Kiburi watakilea, yako kutoyasikia,
Saizi moja mkiwa, nani ataheshimiwa,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

Mughni ayatambua, japo amri katoa,
Yake yadharauliwa, ya kwao wakayazua,
Inachafuka dunia, kwa unafiki kujaa,
Ishi nao matajiri, ila penda mafakiri!

No comments: