Saturday, December 29, 2012

Billa upya kuzaliwa



Mahala tumefikia, budi upya kuzaliwa,
Hilo lisipotokea, janga latunyemelea,
Viraka tukivitia, njiani vitatuumbua,
Bila upya kuzaliwa, naliota jinamizi!

Katiba tumeanzia, na mengine kuingia,
Mali asili kujua, vipi tunajigawia,
Haiwezi kuwa sawa, ilipo na isipokuwa,
Bila upya kuzaliwa, naliota jinamizi!

Tathmini zatakiwa, thamani kuzitambua,
Hesabu kukokotoa, mgawo tukaujua,
Haki ikiangaliwa, salama tutabakia,
Bila upya kuzaliwa, naliota jinamizi!

Uongozi watakiwa, kwanza watu kukomboa,
Kisha ukajinyanyua, hali bora ishakuwa,
Kwanza wanapojilia, tabaka zinashupaa,
Bila upya kuzaliwa, naliota jinamizi!

Usawa huanzia, kwa wanyonge kugawiwa,
Katikati wakikaa, nchi yaweza tulia,
Ila mbali kuachiwa, watakujatuumbua,
Bila upya kuzaliwa, naliota jinamizi!

Muhimu demokrasia, kote ikawakolea,
Ujanja tukiutia, twatafuta majeraha,
Tukitumia hadaa, zitakuja tenguliwa,
Bila upya kuzaliwa, naliota jinamizi!

Yangu ninayawazia, silazimishi yakwa,
Ila ninachokijua, watu wajiamkia,
Kulala wanakataa,  sasa macho wamekuwa,
Bila upya kuzaliwa, naliota jinamizi!

Hili asiyesikia, heri hajatutakia,
Ni kiziwi kuhofiwa, kweli kutoitambua,
Yeye akajiendea, shimoni kwenda tutia,
Bila upya kuzaliwa, naliota jinamizi!


No comments: