Monday, December 24, 2012

Enzi zake zimekwisha

HAKIKA yamefiia, pasina kubwa hatua,
Pazuri kilipoanzia, pabaya chamalizia,
Ukoko waliondoa, na matandu kuachia,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Dunia ina tabia, saburi kuitumia,
Mbio haijakimbia, polepole hutembea,
Wakati ukafikia, pasina kutazamiwa,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Ni ya paukwa pakawa, mwana aliondokea,
Kajenga nyumba kakaa, na vijino vya kupitia,
Cha watu kinapoliwa, cha dhuluma kilikuwa,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Haki njia inajua, giza nuru kwake huwa,
Kila mwenye kuelewa, usaliti huhofia,
Wakati ukifikia, kosa hujisahihishia,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Na kinachochukuliwa, huja kikarudishiwa,
Hakuna cha kupungua, usawa utatimia,
Dhuluma ikanyolewa, kipara ikiachiwa,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Kilichokikichanua, hushidwa toa maua,
Na kinachozaliwa, hakiachi kulemaa,
Kiakili na tabia, na maungo pamwe pia,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Viumbe twajihadaa, yatudanganya dunia,
Mshindi hajatokea, washindwa twajiratua,
Saa zikishafikia, kwa majuto hujutia,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Shari haina wasaa, chunguni inakopikiwa,
Tendo moja latoshea, kwenda huko kupakua,
Sahanini ikitiwa, ukashinwa kujilia,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Nafusi zote zajua, wapi inasimamia,
Na anayelikataa, nakama ajitakia,
Huja yakaezuliwa, yaliyokwishapauliwa,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Moyo wangu nautua, roho ipate tulia,
Nyota usiyojaliwa, huwezi kusafiria,
Nazo za kulazimishia, hatimaye hufubaa,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

Yarabi muelekewa, nadhiri sijajaliwa,
Ila najiondokoea, kuendako wakujua,
Utumwa nimeridhia, wewe nionyeshe njia,
Enzi zake zimekwisha, kichungi chajitembeza !

No comments: