Tuesday, December 11, 2012

Ulinzi wanautaka


Makubwa nimesikia, ya ulinzi kutakiwa,
Mlinzi kukataliwa, kule nyuma kubakia,
Mlindwa hajayajua, yajayo kumtokea ?
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Ulinzi wajivunia, na mapambo kuyatia,
Ila mlinzi nazaa, kituoni kabakia,
Bishara sijaijua, lizukalo kutokea,
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Mlinzi kakataliwa, ulinzi unatakiwa,
Milango amefungiwa, hana pa kujipitia,
Dalili sijaijua, nini inaazimia?
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Idhibati kulemaa, salama haitakuwa,
Waovu hujipitia, saluti wakapigiwa,
Mwizi utamdhania, tena yule asokuwa,
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Walinzi wakigundua, mianya huitumia,
Chao mapema kutwaa, pembeni wakaambaa,
Dola wakaigawia, kidogo cha kubakia,
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Bilioni huchukua, milioni kuwachia,
Nusura huitungua, wakaalika balaa,
Maji wakayaepua, ya moto kwenda kuogea,
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Bandarini huingia, uani wakatokea,
Visovyao kuchukua, wakeenda jiuzia,
Ajira ukiijua, na ujira kuinua!
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Madini huyaachia, angani yakapepea,
Kidogo wakishapewa, kikubwa kwao udhia,
Taifa hudhulumiwa, eti wala si raia,
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Sumu watawauzia, mpate kujichimbia,
Mkenge mkiingia, mbali nanyi watakaa,
Hawatotaka sikia, mkilia kwa makiwa,
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Mafuta wakitoboa, mirija wataitia,
Kisha waanze jinywea, kabla ya kuwaambia,
Siri mkishagundua, watazifua kofia,
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Watazifua kofia, au pengine kuvua ?
Mikono wakachukua, kidogo kuwapakaa,
Ubia wakiwatia, mwache jifaragua,
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

Mwizi anayetwibia, wenyewe tunajijua,
Wengine kusingizia, kitu haitosaidia,
Kweupe twajionea, nje wajilimbikizia,
Ulinzi wanautaka, hawamtaki mlinzi!

No comments: