Tuesday, December 11, 2012

Kidogo huwa ni kingi

AKILI ya kimaskini, kidogo kwake ni kingi,
Ndicho alichobaini, zaidi yana ushungi,
Na neema haioni, rehamaze sio nyingi,
Kidogo huwa ni kingi, akili ya kimsskini!

Hicho hukishangilia, tena akajivunia,
Mbali hakitafikia,ila bado hajajua,
Moja likikunguaa, hali mbaya hurejea,
Kidogo huwa ni kingi, uongozi asojua!

Takwimu asizojua, imani kaziachia,
Ukweli hajaujua, baragumu atumia,
Mbali wakishasikia, sifa za bure hupewa,
Kidogo huwa ni kingi, akili ya kimsskini!

Ukweli wanaojua, kimya kujinyamzia,
Yao wakaangalia, kwa macho ya kusinzia,
Imani wakaondoa, na heshima kuivua,
Kidogo huwa ni kingi, uongozi asojua!

Mengine kwenye dunia, budi mwenyewe kujua,
Watu ukiwaachia, watakulisha hadaa,
Likawa lisiolokuwa, na hewa kutegemea !
Kidogo huwa ni kingi, akili ya kimsskini!

Huanza pakuishia, mwisho kutoufikia,
Ukawa unabomoa, udhani unajegnea,
Na mwishowe kuezua, udhani watia paa,
Kidogo huwa ni kingi, uongozi asojua!

Vijijini tembelea, hata machache masaa,
Mbali kutojisumbua, Ifakara kuingia,
Au hata Pwani pia, na Tanga ya Tanzania,
Kidogo huwa ni kingi, akili ya kimsskini!

Maendeleo ruia, pepesa ikitokea,
Kukohoa na mafua, watesi wameanzia,
Haliwi linalokuwa, hata mbegu hujifia,
Kidogo huwa ni kingi, uongozi asojua!

Mikanda imekaziwa, matumbo ndani kwingia,
Nusura kutodhania, ila viuno kutoa,
Na hili likishakuwa, basi sote twaishilia,
Kidogo huwa ni kingi, akili ya kimsskini!





No comments: