Saturday, December 29, 2012

Mitihani ya dunia


Yataka kuvumilia, mitihani ya dunia,
Kwa uvukayo hatua, imara zaidi kuwa,
Imani kikuingia, utaibana dunia,
Mitihani ya dunia, ni rehema na baraka!

Yataka kujitambua, na kuijua dunia,
Sio kuikimbilia, ajali ikatokea,
Kisha ukaja umia, ndio unakumbukia,
Mitihani ya dunia, darasa hautapewa !

Mwenyewe kujisomea, kawaida inakuwa,
Mwalimu wa  kuyajua, ni viigumu kutokea,
Ualimu watakiwa, mwenyewe kujifanzia,
Mitihani ya dunia, darasa hautapewa !

Dini ukijisomea, lulu huenda ikawa,
Majibi inatumia, ya miaka milenia,
Mbali yanayotokea, na majaribu kujua,
Mitihani ya dunia, darasa hautapewa !

Asili ukiijua, ni hazina inakuwa,
Huku vingi vyachimbiwea, viwezavyo kukufaa,
Katu hautapungukiwa, waweza kujinyanyua,
Mitihani ya dunia, darasa hautapewa !

Kisha ukijitambua, kusoma ukatulia,
Na maswali kuibua, wapi unakotokea,
Kisha ukafaragua, wapi unaelekea,
Mitihani ya dunia, darasa hautapewa !

Hayo ukishayajua, fanaka wakaribiwa,
Kufaulu ndiyo njia, siku ya kutahiniwa,
Mola akitangulia, pasi shiriki kutiwa,
Mitihani ya dunia, darasa hautapewa !

No comments: