Monday, December 10, 2012

Hukerwa na kilio

Mgumu kuvumilia, na subira humpaa,
Kilio ukiangua, huku unaugulia,
Atauona udhia, hataki kukisikia,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Mgonjwa ukitambua, ni mgumu kujijua,
Yeye anaugulia, sio mbwembwe anatia,
Wewe ukimatania, ndugu yangu wakosea,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Waweza kumdhania, ni sanaa anatia,
Uchungu yeye ajua, vipi wewe kuujua,
Hali ungelijaliwa, hapo usingelikaa,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Mwenye njaa hugugumia, mwenye shibe

kafakamia,
Vipi atamuelewa, mkosa asojaliwa,
Tumbo humngurumia, kama ndege ya Ulaya,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Chakula ajionea, ashindwa kukinunua,
Kabaki kukiangalia, kwake sasa ni sanaa,
Wamsimanga raia, mikono atanyanyua,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Palikuwa Malkia, Ufaransa nasikia,
Watu wakamwendea, mikate wanalilia,
Yeye akawashangaa, keki kutokununua,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Shilingi asiyekuwa, vipi maji 'tanunua,
Kiu humashambulia, akatamani kulia,
Mengine ukimwambia, vipi atakuelewa?
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Hatuishi kuzubaa, wnezetu kuporomoa,
Majumba yazidi ng'aa, na shani za motokaa,
Ila mfukoni balaa, senti zinatukimbia,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Haruna Kilewo mbia, zamani aliyekuwa,
Kilio akiangua, hivi sasa kafulia,
Auni aililia, wapi  pa kuingilia,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Mola tunawaombea, mliokuwa mughni,
Mkijatufikiria, tutapata afueni,
Mioyo ikatulia, tudhani tuna thamani,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

No comments: