Saturday, December 29, 2012

Wachawi waende wapi ?


Wana vingi wahofia, nje hawatatokea,
Wana uzi wa ubaya, wenzao wawafumia,
Wana deni wadaiwa, kuwiwa wanahofia,
Wachawi waende wapi, sikukuu hula kwao!

Mila zao za kuvia, hawawezi kuchanua,
Popote wnapokaa, hali huwa zasinyaa,
Sikukuu huchukia, nguvu zao zafifia,
Wachawi waende wapi, sikukuu hula kwao!

Kutabana waishia, bure hawajaijua,
Wakati wautumia, ovyo kwenda jisemea,
Kazi yao kutokuwa, sauti wasipotoa,
Wachawi waende wapi, sikukuu hula kwao!

Si wa kufikiria, jipya wakalizua,
Lao wanalotumia, ukale  limeanzia,
Halina teknolojia, vipi litaendela ?
Wachawi waende wapi, sikukuu hula kwao!

Yao ni ya kusumbua, wala si kusaidia,
Vipi kusherehekea, na misaba wanazaa,
Wanaupenda ukiwa, yalazimu kuulea,
Wachawi waende wapi, sikukuu hula kwao!

Jirani wanapokuwa, yao wanaazimia,
Kuudhi na kusumbua, na furaha kuondoa,
Ukabakia ukiwa, wao wende furahia,
Wachawi waende wapi, sikukuu hula kwao!

No comments: