Monday, December 24, 2012

Wengine

Husemwa waliokuwa, hatujui wangekuwa,
Wengine waliokaa, yao wameyapangia,
Mkazi hujifutua, uungu akajitia,
Wengine wangelikuwa, nchi ingekuwa bora!

Na kila asiyekuwa, yake hatutayajua,
Hadi sikuye ya kuwa, kiwacho kikachipua,
Lake tukajionea, na hesabu kuijua,
Wengine wangelikuwa, nchi ingekuwa bora!

Wapo wanaoshikilia, pasina kitu kuzua,
Hapo wakang'ang'ani, huwa kazi kuwatoa,
Hadi lenu likavia, pasiwe na cha kuchipua,
Wengine wangelikuwa, nchi ingekuwa bora!

Hao watu wa kupewa, vigumu kuyaachia,
Kitu wanakililia, tena wasichotumia,
Chakula wakalilia, kile wasichojilia,
Wengine wangelikuwa, nchi ingekuwa bora!

Kama wanga wanakuwa, gizani wakitembea,
Huku wanuuzia, mambo usiyoyajua,
Ibra ikitokea, uchi utawagundua,
Wengine wangelikuwa, nchi ingekuwa bora!

Matako huyatumia, milango kuisugua,
Dawa wakajichubua, kama hewa wanakuwa,
Wapita bila kujua, mlango wafuramia,
Wengine wangelikuwa, nchi ingekuwa bora!

Hapo kazi kwendelea, uchawi umeshakomaa,
Watu hofu huwatia, ukale kushiikilia,
Hata wanaojichumia, hushindwa cha kujilia,
Wengine wangelikuwa, nchi ingekuwa bora!

Ndivyo ilviyo dunia, mweusi alojaliwa,
Giza lamkimbilia, si yeye kulikimbia,
Afueni kuijua, pengine mwakani ikawa,
Wengine wangelikuwa, nchi ingekuwa bora!

No comments: