Monday, December 10, 2012

Mmepewa mwakiiba ?


Mmepewa mwakiiba ?

HURUMA kawaonea, chenu akawagawia,
Sasa ninashangaa, kuiba mnajitia,
Dhamana mliyopewa, mwataka yenu ikawa ?
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Hapo mlipofikia, kwanza mngetia nia,
Asante mkaitoa, mmshukuru Jalia,
Na chake mkaamua, miliki kuendelea,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Wachamungu mngekua, barazani wanakaa,
Mambo mkajipangia, na umma wote dunia,
Zurufu ikachanua, na harufu  kuenea,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Baraka mwazikimbia, kwa unafiki kuvaa,
Vazi lisilowafaa, tena wahaka lajaa,
Watangulizi walia, kwayo wanayojionea,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Laiti wangelijua, vilabu mngechagua,
Na pombe kuziachia, mitaani kuzagaa,
Uamuzi natambua, ni mwingine ungekuwa,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Mustakimu wakijua, nyie mwaikimbia,
Mkawa magalatia, imani mkafulia,
Wataziua balaa, maskani kukimbia,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Naijua historia, vingine haitakuwa,
Halali haitakuwa, haramu ya kuteua,
Wala kweli kutokuwa, uongo mnaouzua,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Mjeledi wanukia, wa kuchapwas wenye njaa,
Rahisi waliochagua, utata wakakimbia,
Haki wakaiachia, dhuluma kujivunia,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Chake hamtachukua, yeye atawachukua,
Hili mkilitambua, dakika kawaachia,
Fursa kujinasua, pepo yenu kutopaa,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Neema mmejaliwa, na nyie mwaitezea,
Kanga mnaipokea, jora mnalikataa,
Ndizi mnaipokea, mkungu mnaachia?
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Ufukara wa rupia, afadhali inakuwa,
Pia na ule wa njaa, huwa kidogo ubaya,
Ila wa kuwahofia, fukara wa kuongoa,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

Barri mbarikiwa, langu nimeliandaa,
Taa yako langojea, na baraka kulitia,
Utakalo kuja kuwa, umma wako kuufaa,
Mwataka kunmnyang'anya, Rabana

alichowapa ?

No comments: