Saturday, December 29, 2012

Hapa ulipotupita



PUMZI uliyezipewa, nini unajivunia,
Hata ukajipitia, pasina kusalimia,
Hivi zikikuishia, hapo hapo kukwachia ?
Hapa ulipotupita, ni magunia ya mkaa ?

Mwajidanganya  dunia, muonapo mwatembea,
Hizo zaweza kupaa, chini kutoshukia,
Watu wakiwa kinyaa, nao wakawachukia,
Hapa ulipotupita, ni magunia ya mkaa ?

Salama tunaambiwa, si salamu ya dunia,
Juu huko yatokea, yabidi kuheshimiwa,
Hakika ukiitumia, yaweza kukusaidia,
Hapa ulipotupita, ni magunia ya mkaa ?

Rahisi iliyokuwa, bali thamani radhia,
Wengi inawaokoa, mema wakajivunia,
Wewe ukiichezea, inaweza kukuumbua,
Hapa ulipotupita, ni magunia ya mkaa ?

Hebu ivute hatua, na kisha kufikiria,
Nini wajipotezea, kwa watu kusalimia,
Hata wasipoitikia, thawabu wajibebea,
Hapa ulipotupita, ni magunia ya mkaa ?


No comments: