Monday, December 10, 2012

Sisi mbuga za wanyama

HABARI nimesikia, mjini zinatokea,
'Takuja waheshimiwa, kuja kututembelea,
Na wala sio kukaa, kazi kutusaidia,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja  kututembelea?

Vijiji wavibagua, ni mapori vimekuwa,
Kwetu hawawezi kaa, huwa tu wanapitia,
Hali wakajionea, ibaki ilivyokuwa,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja kutuangalia ?

Hamsini yatimia, waendelea udhia,
Sasa tunalikataa, na la kwetu tunatoa,
Kwetu mkijaingia, tutawataka kukaa,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja kutustaajabia?

Tutawataka kukaa, yetu kuzungumzia,
Na fasidi kwa ridhaa, mafungu kuyaachia,
Ysje kwtu kutufaa, tuyaone manufaa,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja  kututembelea?

Matatizo mtajua, mpaswayo kuondoa,
Orodha kuwapangia, kazi hapo kuanzia,
Zito litakalokuwa, kisha mkalianzia,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja kutuangalia ?

Vingine tutakataa, si wanyama tumekua,
Mbugani kuangalia, kisha mkajiendea,
Mkija mje na nia, lipi mwaja kutatua,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja kutustaajabia?

Mamluki kutokuwa, hela mnaomwagiwa,
Kubwabwaja wanaojua, ulevi wakattutia,
Twataka maashallaa, uchamungu walojaa,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja  kututembelea?

Twataka wenye ridhaa, mikono kufunguliwa,
Sio kwao kupendelea, kwengine wakakimbia,
Ubinafsi wamejaa, hawaifai Tanzania,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja kutuangalia ?

Twataka wasionunua, na kanisa kuwanunua,
Kesho watachakachua, amani ikapotea,
Ukasisi wawafaa, huko wakisaidia,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja kutustaajabia?

Huko wakisaidia, ukasisi wawafaa,
Ukabila wakilea, uchifu wakaupewa,
Hawafai Tanzania, ya leo watayalea,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja  kututembelea?

Ukubwa wanaolilia, wito tunawatumia,
Vijijini kujakaa, ya kwetu wakatatua,
Ukabila pasokuwa, na udini kuutia,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja kutuangalia ?

Tumezichoka hadaa, hizo tena si nasaha,
Ujinga tunaulea, wengine kutegemea,
Samaki twawakataa, nyavu tunazingojea,
Sisi mbuga za wanyama, mwaja kutustaajabia?

No comments: