Wednesday, December 5, 2012

W A L A J I

 
 
Walaji mnageuzwa, tena msiojijua,
Vyao vikitengenezwa, mnakuja kutupiwa,
Kila kitu wamefunzwa, kuihadaa dunia,
Mnageuzwa walaji, wasojua kuchagua!
 
Makapu wanachukua, watu wetu kununua,
Wakuu wameteua, kazi hii kufanyiwa,
Wao wamejijakalia, mirija kuichimbia,
Mnageuzwa walaji, wasojua kuchagua!
 
Tonge waliopatiwa, sumu wataitetea,
Uraniamu kukwambia, chumo la kuendelea,
Si la vilema kuzaa, na ugumba kuwatia,
Mnageuzwa walaji, wasojua kuchagua!
 
Mafuta watapakua, wao wasiyotumia,
Mkienda kupikia, utasa mntatanzua,
Hauhitaji ya dawa, nyota ya kijani huwa,
Mnageuzwa walaji, wasojua kuchagua!
 
Amka mkitambua, asubuhi yaingia,
Na unayoandaliwa, salama hayajakuwa,
Kila linalosifiwa, uozandani lajaa,
Mnageuzwa walaji, wasojua kuchagua!
 
Shughulini nako pia, mengi tu yameingia,
Nasaba yasiyokuwa, wala heri kujaliwa,
Mengi yao ni udhia, kama sumu haijawa,
Mnageuzwa walaji, wasojua kuchagua!
 
Hakika vingi vang'aa, ila havitakufaa,
Mifuko vitatoboa, na hasara kuingia,
Mzigo ukachukua, maana usiokuwa,
Mnageuzwa walaji, wasojua kuchagua!
 
Ya walaji milikia, inayotawala dunia,
Hupenda wakutumia, iktisadi kuambaa,
Kila la uongo huzua, ili upate tumia,
Mnageuzwa walaji, wasojua kuchagua!
 

No comments: