Saturday, December 29, 2012

Isije kuwa chooni



WENGINE siwaombei, ila nao kwepushiwa,
Nitakapokuwa hoi, maliwato kuzidiwa,
Ninatoa yangu rai,  huko kutonitokea,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Shetani anakokaa, uchafu kufurahia,
Asikoona kinyaa, na najisi kujinywea,
Huko yasijetokea, pengine nikawahiwa,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Audhubillahi natia, shetani kutosogea,
Najilinda nikitambua, ulinzi nitaupewa,
Na palipo maridhia, mwisho wangu kufikia,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Waipendao dunia, thamani huko watia,
Yao wakayazuia, hata wengine kwingia,
Mimi ninalikataa, la umma nashuhudia,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Tunaowaigizia, hatua wamefikia,
Huko yanayatokea, macho twafunguliwa,
Sinemani yamejaa, ushetani umejaa,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Utajiri wa kung'aa, una tisho la kinyaa,
Thamani yawaishia, utu  unawapotea,
Fedha inaabudiwa, na uungu inapewa,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Dhahabu yaabudiwa, hata roho ikatoa,
Dini sasa imekuwa, madhehebu ya bandia,
Majina wanayopewa, ya uongo na kuzua,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Shea washerehekea, ni ibada zimekuwa,
Watu kutiririkia, mitaani wapagawa,
Hesabu wakisikia, wawe wanashangilia,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Nukta zikifatia, kashfa budi kuzua,
Ujanja unazidia, ila mpya zazaliwa,
Yatosa teknolojia, kwa wale wasiojua,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Vizazi vinajiumbua, kufanyiana ubaya,
Kwa kupotea usawa, na  uzito kulemea,
Haraka waliokuwa, za mkato kutumia,
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !

Mia wakifurahia, elfu wao wanatwaa,
Kila mwenye kudokoa, yuko mwenye kuchimbua,
Adhaniaye apaa, kumbe hivi atembea ?
Isije kuwa chooni, mie pa kuondokea !


No comments: