Saturday, December 29, 2012

Ukijifanya bendera

IKIWA umeamua, ya bendera kuyazua,
Upepo hukuchukua, kushoto hata kulia,
Juu ukakunyanyua, hadi chini kukutia,
Ukijifanya bendera, mwenyewe utajipepea !

Waweza kujisikia, umeikwea dunia,
Hadhi utakayopewa, isiache kukuzua,
Hadi jioni 'kindia,uwe chini washushiwa,
Ukijifanya bendera, mwenyewe utajipepea !

Hali inapotulia, kweli utaheshimiwa,
Na saluti kupigiwa, na watu usiowajua,
Ila wakikuzoea, kitambaa utakuwa,
Ukijifanya bendera, mwenyewe utajipepea !

Nyumayo pasipokuwa, na dola ya kuheshimiwa,
Ila unajitokea, miguu kujiburuzia,
Watu maji hukutia, ukaitwa changudoa,
Ukijifanya bendera, mwenyewe utajipepea !

Hadhari usipotia, mnarani hunyofolewa,
Ukachanwachanwa pia, jalalani kutupiwa,
Sio kitu ulikuwa, ndipo unapojitambua,
Ukijifanya bendera, mwenyewe utajipepea !

Waweza moto kutiwa, pasiwe wa kukuokoa,
Motoni kuteketea, rangi hadi kupotea,
Wasifa uliokuwa, mara sio kitu kuwa,
Ukijifanya bendera, mwenyewe utajipepea !

Waweza kufafiliwa, ufagio mara kuwa,
Vumbi ukalitimua, na buibui kutoa,
Kazi mpya kujaliwa, kazini kujifunzia,
Ukijifanya bendera, mwenyewe utajipepea !

Waweza kunyakuliwa, na mwendambio kichaa,
Shuka akakutumia, usiku kujifunikia,
Maji hautayajua, hadi kuaga dunia,
Ukijifanya bendera, mwenyewe utajipepea !

No comments: