Tuesday, December 11, 2012

Mpira ni kiwanjani


Tanzania yumkini, wanacheza redioni,
Magoli wakabaini, yasiyopo kiwanjani,
Ni nani tumuamini, kama si dakika tisini ?
Mpira ni kiwanjani, hauchezwi gazetini !

wanacheza gazetini, wajenge matumaini,
Wakishuka uwanjani, waliotumwa ubani,
Ni nadra wakawini, kwa maandalizi duni,
Mpira ni kiwanjani, hauchezwi redioni!

Tuwafupi fikirani, na mpango si makini,
Na usomi siudhani, unaoneza thamani,
Hajasoma Platini, ona alivyo makini,
Mpira ni kiwanjani, mwacheza kwenye tivii?

Viongozi wa tumboni, wanatuacha jangwani,
Katiba tuibaini, wapenzi kuwathamini,
Michezo isiwe duni, kwa uongozi yakini,
Mpira ni kiwanjani, hauchezwi gazetini !

Ni aibu tiviini, kujiona uwanjani,
Kama vile zoezini, wakubwa wenye thamani,
Muundo tusipoauni, tutaozea nyumbani,
Mpira ni kiwanjani, hauchezwi redioni!

Vipaji tele nchini, nani wa kuvithamini,
Wakubwa wanazaini, wa kwao sio kundini,
Vipi vyetu kuthamini, vikaingia nyotani?
Mpira ni kiwanjani, mwacheza kwenye tivii?

Ubinafsi waamini, majumbani na njiani,
Vipi tutawaamini, waushike usukani,
Tuwatafute amini, spoti wakadhamini,
Mpira ni kiwanjani, hauchezwi gazetini !

Mijitoto ya mjini, wanaishusha thamani,
Wameingia vitini, ili yao kuyawini,
Si mazuri kuyawini, tusifike duniani,
Mpira ni kiwanjani, hauchezwi redioni!

Wanaifanza hisani, tuwachangie mapeni,
Wakitia mifukoni, wale na wana ndani,
Kazi zao hatuoni, tutafulia mwakani,
Mpira ni kiwanjani, mwacheza kwenye tivii?

Amkeni majinuni, michezo ina thamani,
Ikiongozwa makini, tutashinda umaskini,
Tukiachia wahuni, twaingia mkengeni,
Mpira ni kiwanjani, hauchezwi gazetini !

Amkeni vijijini, timu zenu mbaini,
Wachache wakijawini, watajenga vijijini,
Hadhi mkaibaini, kimataifa yakini,
Mpira ni kiwanjani, hauchezwi redioni!

Viwanja kavijengeni, na ya kukaa mabweni,
Mwingie mashindanoni, na vijana wa mjini,
Haitafika mwakani, kiwango mtakiwni,
Mpira ni kiwanjani, mwacheza kwenye tivii?



No comments: