Monday, December 24, 2012

Wapitao watapita


Wapo waliozaliwa, njia hii kupitia,
Yao wakatunukiwa, na mbele kuendelea,
Huwafuta historia, pasina jiwe kupewa,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

Wengi watajipitia, hivyo hivyo kujizoa,
Lao kuliangalia, ya wengine yakivia,
Matatizo kuachia, miongo kuendelea,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

Ya kwao watayapewa, dunia kufurahia,
Ziada hawatapewa, kavukavu huzolewa,
Kwenye kona kutupiwa, gizani kulikouwa,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

Wapo wataochanua, kama vile ni maua,
Kwa vyeo na ushujaa, katika hii dunia,
Wakubwa kutumikia, hata kwa yenye ubaya,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

Uongo watauzua, na wengine kuwaua,
Takirima wakapewa, kwenda kula na jamaa,
Siku ikifikia, huwa sio  historia,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

Wale wanaojijua, kutumiwa wakataa,
Rabuka huwaandaa, mitihani kuivaa,
Kidede kuwanyanyua, goli wakajifungia,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

Vizazi hushangilia, majina yakabakia,
Watunzi wakatambua, na nukuu kuzitia,
Vitabu mkifungua, hamtoacha wajua,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

Huukubali ukiwa, yenu yapate jaliwa,
Wakaishi kwenye njaa, ili shibe kutowakimbia,
Mateso huvumilia, ili msikose furaha,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

Fikira mkijaliwa, hili mtalitambua,
Katika hii dunia, hivi sasa ni sanaa,
Uongo mnachorewa, na ukweli wafukiwa,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

Macho mtakapokuwa, ujanja mtaujua,
Waongo kuwagundua, kumbe pamoja mwakaa,
Yao mkayachagua, ubwabwani kuyatoa,
Wapitao watapita, pasiwe wa kukumbukwa.

No comments: