Tuesday, December 11, 2012

Pumnba ukizipepeta

Nafaka hazitakuwa, pumba ukizichengua,
Hata pia kupembua, yakinifu kuijua,
Mchecheto huuvaa, hakiwi kisichokuwa,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

Pumba ukishajaliwa, mapumba yatabakia,
Nafaka adimu kuwa, huwezi kujiuzia,
Ila inapotakiwa, kuku kwenda kulishia,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

Pumba ukiipambua, na thamani kuitia,
Pumba tu itabakia, vingine haitakuwa,
Daraja lakadiriwa, zaidi haitafikia,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

Pumba ukichekechea, hadhi haitajongea,
Pale pale hubakia, asili kuililia,
Hata unapojaliwa, zuri dhahabu gunia,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

Kwenye dhahabu gunia, pumba ukamiminia,
Kugeuka ni nazaa, nafaka ikatokea,
Palepale husalia, hadhi yake imepewa,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

Pumba nchi ikipewa, hadi kote kuenea,
Watu watachakachua, kwenye nafaka kutia,
Ubora ukafifia, kwa mchele na bidhaa,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

Hadhi watajionea, ni kubwa wamefikia,
Hapo hapo hubakia, juu kutojionea,
Maktaimu wakatia, nchi nyuma kubakia,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

Nje wasikoyajua, mazuri kujionea,
Wakabaki wasikia, na tivii kupapua,
Hadhi watajisifia, ya chini iliyokuwa,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

Akili zitafikia, ukomo uliopewa,
Zaidi zitapwelea, bora kutoyaelewa,
Kulalama kwao kuwa, ada ya asiyelijua,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

Zitwange na kutwangua, usafi zitakataa,
Zioshe na kuagua, usafi hazitajua,
Asili huililia, imeamua dunia,
Pumba ukizipepeta, bado unapata pumba!

No comments: